TIMU YA SIMBA ILIVYOJIBU MASWALI MAGUMU LIBYA

 

TIMU YA SIMBA ILIVYOJIBU MASWALI MAGUMU LIBYA

Simba SC imekutana na mtihani wa kwanza kimataifa msimu huu uliokuwa na majibu magumu ambayo mwisho wa siku imeondoka na kitu chenye faida.


Matokeo ya 0-0 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika ugenini dhidi ya Al Ahli Tripoli ni faida kwa Simba, lakini pia ni mtego endapo tu itaruhusu bao mechi ya marudiano nyumbani ikitokea 1-1 kwani sheria ya bao la ugenini itatumika kuamua matokeo ya jumla na kujikuta nje ya mashindano.


Ikumbukwe kwamba Al Ahli Tripoli iliyoiondosha Uhamiaji ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 5-1 katika michezo miwili ya hatua ya awali kunako michuano hiyo, juzi Jumapili ilipambana na Simba nyumbani kwao na kubanwa.


Licha ya kufanya mashambulizi mengi katika mchezo huo, lakini wenyeji waliishia kutotikisa nyavu za Simba kitu ambacho mashabiki wao kiliwakakasirisha na kufanya vurugu.


Kilichotokea ndani ya uwanja, kwa namna moja ama nyingine kimekuwa faida kwa Simba, lakini kazi bado haijaisha.


Kuna mchezo wa marudiano utakaochezwa Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo Simba inahitaji ushindi wa aina yoyote ili kufuzu hatua ya makundi.


Kabla ya kuuendea mchezo wa marudiano, kuna vitu vilijitokeza jana ambavyo vinatoa picha nzima ya nini kilichopo mbele.


NIDHAMU YA ULINZI


Chini ya nahodha Mohamed Hussein, safu ya ulinzi ya Simba ilifanya kazi kubwa kuzuia mashambulizi ya Al Ahli Tripoli.


Al Ahli Tripoli ambayo ilikuwa na wachezaji hatari eneo la ushambuliaji kama Agostinho Cristóvão Paciência maarufu Mabululu, lakini hawakufanikiwa kuipenya ngome ya Simba.


Ukiachana na Mohamed Hussein upande wa kushoto, lakini Shomari Kapombe naye alihakikisha upande wa ulinzi kulia anapambana kwa namna yake.


Pale katikati, Che Malone Fondoh na Abdulrzack Hamza nao walikuwa na utulivu mkubwa kiasi kwamba walizima mashambulizi yote ya Al Ahli Tripoli ambayo muda mwingi ililishambulia lango la Simba.


Ni wazi Kocha Fadlu Davids amepata pacha katika eneo la beki wa kati ambapo Che Malone na Abdulrzack wanacheza kwa kuelewana sana tangu kuanza kwa msimu huu.


Abdulrazack ambaye ni usajili mpya, ni beki mzawa aliyeonyesha Simba hawakukosea kumtoa SuperSport United ya Afrika Kusini na kumshusha Msimbazi.


Ukiachana na kazi kubwa iliyofanywa na mabeki, lakini huwezi kuacha kutoa sifa kwa kipa wa Simba, Moussa Camara ambaye alikuwa imara katika eneo lake la golini.


Camara ambaye kwa sasa anaonekana kuichukua nafasi ya kipa namba moja kikosini hapo, aliokoa hatari zaidi ya tatu zilizoelekezwa langoni kwake zikiwemo mbili za Mabululu na Ahmed Kraouaa.


SHIDA IPO HAPA


Licha ya kwamba Simba iliingia uwanjani na kucheza zaidi soka la kulinda lango lao, lakini kuna sehemu ilionekana kuwa na shida kitu ambacho Kocha Fadlu Davids anapaswa kwenda kukifanyia kazi.


Eneo la ulinzi na kiungo la Simba lilicheza vizuri, lakini shida ilikuwepo katika kushambulia wachezaji waliocheza eneo hilo hawakuwa na utulivu.


Joshua Mutale mapema tu dakika ya kwanza alipata nafasi ya kulishambulia lango la Al Ahli Tripoli, lakini mpira wake wa mwisho hakuupiga vizuri licha ya kwamba ilikuwa faida kwa Simba kupata kona.


Mutale hakuwa na siku nzuri kutokana na kupoteza mipira mingi kwani hata nafasi hiyo aliyoipata alilazimisha kufunga akiwa eneo gumu zaidi.


Pia winga Edwin Balua akiwa na mpira pembeni kidogo mwa boksi la Al Ahli Tripoli, alishindwa kuwa mtulivu hadi beki akaja kuokoa hatari.


ATEBA ANA KITU


Ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa mshambuliaji wa Simba, Leonel Ateba ambaye amesajiliwa dakika za mwisho msimu huu kuimarisha eneo hilo la ushambuliaji.


Ateba aliyecheza kwa takribani dakika 70, aliiongoza safu ya ushambuliaji ya Simba akiwasumbua mabeki wa Al Ahli Tripoli. Utumaiaji mkubwa wa nguvu ilikuwa silaha yake kiasi cha kuwafanya mabeki wa Al Ahli Tripoli kuwa naye makini muda mwingi.


Katika mchezo wake wa kwanza wa kimashindano na kile alichokionyesha ni wazi kwamba akiendelea hivi anaweza kuwa suluhisho la eneo la ushambuliaji ambalo Simba linawatesa.


MAVAMBO YULEYULE


Katika eneo la kiungo, Debora Fernades Mavambo ameendelea kuonyesha ubora wake tangu siku ya kwanza kuichezea Simba.


Kiungo huyo ambaye ni msimu wake wa kwanza ndani ya Simba, juzi alicheza vizuri katika eneo lake la kiungo cha kati akisaidia kukaba na kupandisha mashambulizi kama ambavyo amekuwa akifanya siku zote.


Uimara wake unaendelea kudhihirisha kwamba tayari amejihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.


FADLU AMEFANIKIWA


Unaweza kusema Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids mpaka sasa amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuitengeneza timu hiyo kushindana kwa namna yoyote ile.


Al Ahli Tripoli ambayo katika mechi tatu za nyuma mfululizo ilifanikiwa kufunga jumla ya mabao sita, juzi ilisimamishwa na Simba.


Kusimamishwa huko kwa Al Ahli Tripoli kunakwenda sambamba na mbinu za Fadlu ambaye tangu ametua Simba msimu huu amekuwa akitumia mfumo wa kuimarisha zaidi ulinzi akiwaweka viungo wakabaji wawili.


Katika mchezo wa juzi, Fadlu kwenye eneo hilo aliwatumia Mavambo na Yusuph Kagoma. Ikumbukwe kwamba, anapotumia viungo hao, anahakikisha mmoja anakuwa na kazi mbili, kukaba na kusaidia mashambulizi kitu ambacho Mavambo amekuwa akikifanya.


WAKUCHUNGWA


Mpaka dakika 90 zinamalizika juzi, watu wengi watakuwa wamepata picha halisi ya Al Ahli Tripoli ambacho awali pengine hakikufahamika kutokana na kutoifuatilia kwa undani zaidi timu hiyo.


Juzi kuna wachezaji watatu wa eneo la ushambuliaji la Al Ahli Tripoli walioonekana kuisumbua sana safu ya ulinzi ya Simba ambayo uimara wao uliwaokoa.


Washambuliaji Mabululu na Ahmed Kraouaa, ni kati ya wachezaji wanaopaswa kuchungwa zaidi kutokana na kile walichokifanya juzi.


Wawili hao walikabidhiwa mikoba ya kuiongoza safu ya ushambuliaji na wote walionyesha wana kitu kwani Mabululu alifanya mashambulizi mawili ya hatari, huku Kraouaa akionekana kuwa hatari kwa mipira ya vichwa kwani kichwa chake kimoja alichopiga dakika ya 90+3 kiligonga mwamba wa pembeni ikawa salama kwa Simba.


Naye kiungo mshambuliaji Mourad Hedhli ni mtu wa kuangaliwa zaidi kama ilivyo kwa nahodha Muaid Ellafi anayecheza nafasi ya winga ya kushoto.


Ellafi ni hatari akiwa na mpira kwani anamlazimisha beki kuingia naye kwenye boksi ili tu afanyiwe faulo itokee pembeni.


Ilibaki kidogo afanikiwe katika hilo baada ya kumtoka Che Malone dakika ya 73 ambapo walipelekana kutoka pembeni hadi ndani ya boksi lakini Che Malone akafanikiwa kuucheza mpira na kuwa kona ingawa wachezaji wa Al Ahli Tripoli walimlalamikia mwamuzi kwamba nyota huyo amefanyiwa faulo iliyopaswa kuwa penalti.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad