MCHEZO WA CBE NA YANGA UMENIKUMBUSHA MWAKA 1947

 

MCHEZO WA CBE NA YANGA UMENIKUMBUSHA MWAKA 1947

Nimekumbuka zamani. Mwaka ‘arobaini na sabaa’. Pambano la CBE dhidi ya Yanga lililochezwa juzi pale Addis Ababa. Futi nyingi juu kutoka usawa wa bahari. Mashabiki wa Yanga hawakuridhishwa na matokeo, ingawa waliyakubali. Walishinda bao 1-0 ugenini.


Zamani wakati ule timu za Tanzania zikipangwa na timu za Misri katika hatua za awali. Malalamiko yalikuwa ni namna gani CAF walikuwa wanazionea timu za Tanzania kwa kuzipanga na timu ngumu za Misri. Kina Al Ahly, Zamalek, Ismailia na wengineo ambao walikuwa wagumu kutoka Afrika Kaskazini. Kumbe tulikuwa hatuonewi.


Tulipaswa kusogea mahali na sisi kuwa katika nafasi hiyo. Ina maana mbili. Kwanza kusogea kwa kufanya vizuri katika michuano ya CAF katika namna ya kuwakwepa hawa wababe. Ilipaswa wote tuonekane kuwa katika daraja moja ili tukwepane. Ndicho ambacho kimetokea kwa sasa. Baada ya Simba na Yanga kufanya vema katika michuano ya CAF haiwezekani kwa Simba na Yanga kupangwa na Al Ahly katika hatua za awali kama ambavyo Gor Mahia amepangiwa Al Ahly katika hatua hizo.


Lakini ukweli haujifichi. Mashabiki wa Yanga juzi hawajaridhishwa sana na walichokiona uwanjani kwa sababu waliamini walipaswa kwenda Ethiopia na kushinda mabao mengi dhidi ya bingwa wa Ethiopia. Ni kama ambavyo miaka kadhaa nyuma mashabiki wa Al Ahly waliamini kwamba timu yao ilipaswa kuja Dar es Salaam na kushinda mabao mengi.


Kama sio kushinda mabao mengi basi waliamini walipaswa kuja Dar es Salaam na kupata matokeo. Ni kama ambavyo Yanga walikuwa wanajisikia juzi. Haishangazi kuona lawama zao zipo kwa Prince Dube. Yanga hawajadiliani habari ya ushindi ugenini. Zamani ingekuwa habari kubwa, lakini kwa sasa ni habari ya kawaida. Wanachoshangaa ni namna gani hawajafunga mabao mengi.


Kumbe CAF walikuwa hawatuonei. Kile kile ambacho kilikuwa kinatutokea sisi miaka ile ndicho ambacho kimewatokea rafiki zetu CBE juzi. Yanga walikuwa ugenini, lakini walikuwa wanacheza kama vile wapo nyumbani. Wao ndio walikuwa na mpira na wao ndio walikuwa na uamuzi wa mechi mkononi. Dhidi ya bingwa wa nchi katika ardhi yake.


Na wakati mpira ukiendelea namna ambavyo Yanga walikuwa wanacheza ilikuwa wazi ungejua kuwa katika mechi ya pili Yanga wangekuwa nyumbani na kumaliza kazi. Ni kama zamani tu ambapo kama Al Ahly au Zamalek angeshinda bao moja au kutoka sare Dar es Salaam basi tulijua timu yetu ingetolewa wiki moja baadaye pale Cairo.


Hadi wakati huu naandika makala hii sijajua ambacho Simba ingeweza kukifanya pale Tripoli Libya, lakini ni wazi kwamba timu zetu zimesogea mbele hatua kadhaa tofauti na kule ambako tulikuwa. Pesa imewekwa katika mpira wetu. Nadhani wachezaji wa kigeni wametusaidia kuwa katika hatua hii. Ingefurahisha kama wachezaji wetu wazawa wangekuwa wamewezesha hili lakini ukweli ni kwamba noti zetu kwa wachezaji wa kigeni zimesababisha hili.


Na sasa matarajio yamekwenda juu kiasi kwamba habari sio tu kuwatoa CBE bali kwenda katika makundi na kushika nafasi ya juu kwa ajili ya kwenda robo fainali. Bahati mbaya katika hili Azam ndio ambao wametuangusha. Kwanini walitolewa katika hatua ya awali na timu kutoka Rwanda? Imeshangaza.


Ndani ya uwanja. Yanga walikuwa bora. Kuna tatizo kwa Prince Dube. Anapoteza nafasi nyingi uwanjani. Yeye ndio alikuwa shujaa wa mechi kwa bao la ushindi, lakini angeweza kuondoka na mpira kama angekuwa makini. Wakati mwingine ni kwa sababu tumekariri. Kama nafasi zile angekuwa anapoteza Clement Mzize tungekuwa tunaongea habari nyingine.


Ndani ya uwanja pia Stephane Aziz Ki inabidi atazamwe kwa jicho jingine. Ni mtoto wa kishua. Mama yake ana kazi nzuri kule Afrika Magharibi. Wakati mwingine anaufanyia mpira masikhara mengi. Huwa tunamtazama Aziz katika matukio mazuri ya kuamua mechi. Hatumtazami namna anavyofanya masikhara na mpira. Anapoteza mipira ovyo.


Aziz anakosa ukomavu wa akili. Anawasaidia sana Yanga, lakini hapo hapo ni mchezaji anayepoteza mipira sana. Haonyeshi umakini mkubwa katika maeneo muhimu. Wakati mwingine anacheza kwa kile kitu Waingereza wanaita ‘mood’. Inategemea namna anavyojisikia kwa siku hiyo.


Miguel Gamondi anapaswa kuchukua uamuzi mgumu. Katika mechi za kimataifa ameshakariri kikosi chake katika utatu wa Pacome Zouzoua, Aziz Ki na Maxi Nzengeli. Ni wakati wa Clatous Chama kuanza kuingia katika kikosi hiki moja kwa moja. Sidhani kama Chama atakuwa ana furaha kukaa katika benchi huku Aziz akifanya masikhara uwanjani.


Hadi sasa Chama amekuwa akianza katika zile mechi ambazo zinaonekana hazina umuhimu sana. Mfano ni marudiano dhidi ya Vital’O. Muda si mrefu atahitaji kuanza katika mechi zenye mikiki ambazo zinaamua hatima ya Yanga.


Hata hivyo, uwepo wa Chama uwanjani unawarahisishia sana kazi washambuliaji kwa vile miaka yote tangu yupo Simba na hata anapokuwa na timu ya taifa ya Zambia, Chama ameamua sifa zake kuwa ni kuwatengenezea mabao wenzake.


Anafanya kazi rahisi tu uwanjani ya nipe nikupe. Ukiwa mjanja wa kufika kwenye nafasi basi Chama atakufanya ubaki unatazamana na kipa mara kwa mara ukiwa na mpira. Tazama bao ambalo Clement Mzize alifunga dhidi ya Azam katika fainali ya Ngao ya Jamii.


Ilikuwa ni akili ya kufanya kitu rahisi ambayo Chama alikuwa nayo iliyompa lile bao Mzize. Katika mpira wa miguu makocha wengi wanaamini kuwa kazi ngumu uwanjani ni kufanya kitu rahisi.


Kuna ukweli fulani ambao mabeki watatu wa Yanga, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Bacca wanauonyesha kwa wachezaji wetu wazawa ambao ni mchezaji kutotengeneza pengo kubwa la ubora baina yako na mwenzako ambaye unashindania naye nafasi ya kucheza.


Juzi Miguel Gamondi alilazimika kutumia mfumo wa kutumia mabeki wa kati watatu kwa pamoja kwa vile alikuwa na wasiwasi na hali ya ufiti wa beki wa kulia Yao Kouassi Attohoula.


Na hata katika mechi ambazo Bakari Mwamnyeto huwa haanzi kikosini, Gamondi mara nyingi amekuwa akimuingiza kutokea benchi kwa tafsiri ya harakaharaka kuwa hataki kupoteza ubora wake na hili hufanyika hata katika kikosi cha Taifa Stars.


Mwamnyeto, Job na Bacca hawajapishana sana ubora na ndio maana makocha hawako tayari kuona mmoja anasotea benchi kwa muda mrefu ili asimpoteze. Haiji kwa bahati mbaya au upendeleo.


Yote haya yanabebwa na hoja moja ambayo nimeigusia hapo juu kuwa kuna fedha imewekwa kwenye soka letu ambayo inatoa kiburi kwa makocha na timu zetu kushindana na miamba ya Afrika.


Jumanne iliyopita, Taifa Stars ilikuwa Ivory Coast kucheza na Guinea katika mechi ya kuwania kufuzu ushiriki wa Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 ambayo ilishinda kwa mabao 2-1.


Muda mfupi baada ya mechi kumalizika, Yanga ikasafirisha haraka wachezaji wake saba ambao waliwahi kufika Ethiopia na kupumzika zao hotelini kabla hata ya msafara wao kutoka Tanzania haujafika kule. Watani wao Simba nao wakafanya hivyohivyo kwa kuwasafirisha wachezaji wao wanne kuwahi Libya kabla hata kikosi chao hakijafika nchini humo.


Zamani wachezaji wangelazimika kurudi hadi nyumbani Tanzania kisha timu zikaanza kuhangaikia namna ya kuwasafirisha kwenda ambako watacheza mechi. Lakini nguvu ya fedha imerahisisha mambo. Sasa wanaunganisha juu kwa juu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad