Simba imewashtukia Waarabu kutokana na kuizuia kupata bao lolote, kisha wenyewe kuzipiga uwanjani na kocha wa Wekundu hao, Fadlu Davids akasisitiza anataka ushindi wa kishindo nyumbani.
Hiyo ilikuwa juzi katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa nchini Libya ambapo ulipomalizika vurugu kubwa zilizuka za mashabiki huku wachezaji wakimzonga mwamuzi.
Jumapili, wiki hii, Simba itacheza na Al Ahly Tripoli ya Libya katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika utakochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar ambao utaamua nani atasonga mbele.
Baada ya mchezo wa juzi, Simba ilibaki jijini Tripoli ambapo jana ilifanya mazoezi kisha leo usiku itaanza safari ya kurudi Dar es Salaam ikitarajiwa kuingia nchini kesho Jumatano alfajiri tayari kwa maandalizi ya mchezo huo wa marudiano.
Huku nyuma, kocha wa Simba, Fadlu ameliambia Mwanaspoti kuwa mchezo uliopita umewapa uhalisia wa ubora wa wapinzani wao na kwamba sasa wanajipanga kwenda kwa Mkapa kuhakikisha wanapata ushindi mkubwa nyumbani kwani tayari wameshtukia mbinu za Walibya hao.
Fadlu alisema wanarudi nyumbani ambapo watakuwa na mazoezi mengi ya kuhakikisha timu inapata ushindi muhimu baada ya suluhu ya ugenini, huku kazi kubwa ikiwa ni kulinda wasiruhusu bao kwani anafahamu wapinzani wao watakuja kwa kushambulia kutafuta bao ili wapate nguvu mpya.
“Hii mechi ya kwanza imekwisha, kila timu ina nafasi ndani ya dakika 90 zijazo tutakazokuwa nyumbani, tunatakiwa kuwa na ubora wa kuamua mechi kwa kushinda, hili ndio muhimu kwetu,” alisema Fadlu na kuongeza:
“Sare isiyo ya mabao na tukiwa tunarudi nyumbani inatutaka kuwa makini, nawapongeza wachezaji wangu hasa wa eneo la ulinzi walikuwa na dakika 90 bora lakini tunatakiwa kucheza kwa umakini kuliko mechi iliyopita, kama tukifanya makosa ya kuruhusu bao hasa tukiwa bado hatujapata mabao itatuweka kwenye presha.”
AMTAJA ATEBA
Juzi Jumapili mshambuliaji Leonel Ateba alicheza mechi yake ya kwanza ya kimashindano tangu ajiunge na Simba msimu huu akitokea USM Alger huku akionekana ana kitu cha kufanya ndani ya uwanja endapo akipata muda zaidi wa kucheza.
Hata hivyo, Ateba ambaye aliiongoza safu ya ushambuliaji ya Simba, kwa ujumla walishindwa kuzitumia nafasi walizotengeneza kitu ambacho Fadlu amesema wanahitaji kulifanyia kazi jambo hilo.
Katika eneo hilo la ushambuliaji, mbali na Ateba, pia Edwin Balua, Jean Charles Ahoua na Steven Mukwala walianza kikosi cha kwanza huku wakipata nafasi kadhaa za kufunga na kushindwa kuzitumia vizuri.
“Mchezo wa nyumbani tutakuwa na kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha tunatumia nafasi za kufunga, nilisema awali mechi kama hizi kubwa hazina nafasi nyingi za kufunga, tunatakiwa kujiandaa kutumia nafasi hizo chache tutakazozitengeneza.
“Mechi ya jana (juzi) tulitengeneza nafasi hasa kipindi cha kwanza lakini bahati mbaya tulikosa ubora wa kuzigeuza kuwa mabao,” alisema Fadlu.
Fadlu alitoa tahadhari akisema wachezaji wake wanatakiwa kuendeleza ubora wa kucheza kwa utulivu kwenye safu ya ulinzi ili kuhakikisha hawaruhusu bao lolote wakiwa nyumbani.
Kocha huyo Msauzi amewataka mashabiki wa Simba kuja kwa wingi uwanjani kuwathibitishia Waarabu hao kuwa hata wao wanaweza kuujaza uwanja wenye mashabiki 60,000 kuliko ule wao uliojaza mashabiki 45,000.
“Tulikuwa na dakika 90 ngumu mbele ya mashabiki wao 45,000, naamini sisi mashabiki wetu watakuja kuwalipa kwa kuujaza uwanja wenye watu 60,000 ili vijana wetu wawe na nguvu uwanjani.”
Simba inasaka nafasi ya kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo mara ya mwisho kushiriki michuano hiyo ilikuwa msimu wa 2021/22 ilipoishia hatua ya robo fainali ikiondoshwa na Orlando Pirates kwa penalti 4-3. Al Ahli Tripoli katika msimu huo waliishia nusu fainali ambapo pia walifungwa na Orlando Pirates jumla ya mabao 2-1.