Mshambuliaji Kennedy Musonda bado yupo Yanga baada ya kujumuishwa kwenye kikosi cha msimu ujao, huku mshambuliaji mpya Prince Dube akitajwa kuhusika.
Awali, Yanga ni kama ilikuwa inafikiria kuachana na washambuliaji wawili Musonda na Joseph Guede, lakini baadae wakambakisha Musonda huku Guede akipelekwa Singida Black Stars.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema, mabosi wa klabu hiyo wamekubaliana kwamba Musonda abakishwe kwenye kikosi hicho, kutokana na kutokuwa na rekodi kubwa ya majeraha ingawa changamoto kwake ilikuwa idadi ya mabao ambayo ameyafunga ndani ya timu hiyo kwa miaka miwili.
"Viongozi wa Yanga wameona wambakishe Musonda ili awe sehemu ya kikosi hicho kuweza kuisaidia timu hiyo kama mshambuliaji wao mpya Prince Dube ataendelea na rekodi yake kuwa majeraha."
Dube aliyesajiliwa na Yanga kwenye dirisha hili la usajili, akiwa na Azam FC amekuwa na rekodi ya kukaa nje mara kwa mara kutokana na majeraha hatua ambayo klabu yake mpya imeamua kujiandaa sawasawa.
"Ndio Musonda atabaki, tumemuongezea mwaka mmoja zaidi, unajua tunatakiwa kujiandaa kama Dube atakuwa na majeraha yake ya mara kwa mara," alisema bosi huyo.
"Kuchelewa kwake kujiunga na timu aliomba ruhusa alikuwa na mambo yake binafsi,nadhani atakuwa hapa kabla ya timu kuondoka kwenda Kambi ya nje ya nchi."
Yanga sasa imeshakamilisha idadi ya wachezaji 12 wa kigeni ambao wanatakiwa kisheria, hivyo unaweza kusema kwa msimu huu wameshamaliza nafasi za wachezaji wa kigeni kama hawatabadili maamuzi.
Djigui Diara, Chadrack Boka, Kouasi Yao, Pacome Zouzoua, Aziz Ki, Clatous Chama, Kennedy Musonda, Jean Baleke, Maxi Nzengeli, Prince Dube, Khalid Aucho na Duke Abuya ndiyo wachezaji wao wa kimataifa.
NAFASI YA MUSONDA ILIPATIKANA HAPA
Yanga sasa imeamua kuwa na washambuliaji wa kigeni watatu huku nafasi ya Musonda ikipatikana kwa mpango wao wa kumuondoa Gift Freddy, ambaye msimu uliopita ndio ulikuwa wa kwanza na hakupata nafasi ya kucheza.
Taarifa za ndani zinasema;"Ni ngumu Gift kubaki kwani safu ya ulinzi Yanga iko imara na Mwamnyeto tayari alishaongeza mkataba hivyo, ugumu wa kupata nafasi unazidi kuongezeka kwake,"
"Msimu ujao tunahitaji kuwa imara zaidi hasa eneo la kufunga ili kuweza kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ndio maana tunaongeza majembe hasa upande wa washambuliaji."
Hivyo msimu ujao Yanga itakuwa na washambuliaji wanne ambao msimu uliopita walimaliza na rekodi zao za kufunga mabao ambapo Clement Mzize (6), Kennedy Musonda (4), Prince Dube (7) na Jean Baleke (8).