HATIMAYE Simba Wafanikisha Kumbakiza KIBU Denis, Apewa Kitita Hichi cha Fedha.....

 

HATIMAYE Simba Wafanikisha Kumbakiza KIBU Denis, Apewa Kitita Hichi cha Fedha.....

Baada ya mvutano mkubwa kati ya klabu ya Simba na mshambuliaji wake Kibu Denis juu ya kusaini mkataba mpya, taarifa zinasema kuwa pande hizo mbili hatimaye zimefikia makubaliano na nyota huyo atasalia klabuni hapo kwa misimu miwili zaidi.


Taarifa ya uhakika zinasema Kibu kupitia kwa wawakilishi wake amekubali kusaini mkataba mpya wa miaka miwili wenye thamini ya shilingi milioni 300 (sawa na milioni 150 kwa kila mwaka).


Mmoja wa watu wa karibu wa mchezaji huyo aliiambia Nipashe jana kuwa licha ya Yanga kuwasilisha ofa yao, Kibu ameamua kusalia Msimbazi baada ya kukubaliana dau na nyongeza kubwa ya mshahara wake.


"Nikwambie tu kuwa Kibu ameamua kusalia Simba mpaka Juni 2026, amesalia kwa ada ya uhamisho Sh. milioni 300, amepewa Sh.milioni 150 kwanza na nusu nyingine atamaliziwa," alisema mtoa taarifa huyo.


Alisema ni kweli klabu ya Yanga ilikuwa imemwekea Kibu dau la Sh. milioni 350 na ilikuwa tayari kutoa zaidi ya hiyo, lakini ongezeko hilo limekuja wakati tayari mchezaji huyo ameshasaini mkataba wa awali na Simba.


"Siyo uongo, kuna watu wanasema sijui meneja wake alikuwa akiitaja Yanga kumtaka ili kumpandisha thamani, si kweli, jamaa kweli walikuwa wanamhitaji na ilibaki kidogo tu.


"Kilichosababisha ishindikane ni kwamba, Yanga ilitoa ofa ya Sh. milioni 350, lakini ongezeko hilo lilionekana ni dogo kwa mchezaji na kuona ni bora abaki kwenye klabu ambayo ameizoea. Baadaye Yanga ikaja na ofa nyingine nono zaidi ya hiyo, lakini kwa bahati mbaya ilikuwa imeshachelewa kwani mchezaji alikuwa ameshasaini mkataba wa awali na klabu yake ya zamani, hapo ndipo mchezo ulipoishia, kama ofa ya pili ingeletwa mapema kabla hajasaini Simba saa hizi tungekuwa tunaongea mengine, jamaa amebaki Simba," alisema mtu huyo wa karibu na Kibu.


Alisema, katika mkataba wake huo mpya, mshahara wake umepanda kutoka Shilingi milioni nane mpaka shilingi milioni 15 kwa mwezi kiasi ambacho Kibu alikihitaji.


Winga huyo ambaye hucheza kama mshambuliaji wa kati, alijiunga na Simba 2021, akitokea Mbeya City na anamaliza mkataba wake wa awali mwishoni mwa msimu huu.


Alipoulizwa juu ya taarifa hiyo, Meneja Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema Simba wapomakini kwenye masuala yao ya usajili na hakuna mchezaji wanayemuhitaji ataondoka Simba na kujiunga na klabu nyingine ya hapa nyumbani.


Alisema uongozi utatoa taarifa kama kuna jambo lolote limefanyika kuhusiana na usajili.


Wakati huo huo, Simba ipo kwenye mpango wa kumsajili golikipa wa kimataifa wa Cameroon, Joseph Fabrice Ondoa ambaye anacheza soka lake nchini Ufaransa iwapo kipa wake, Ayoub Lakred ataamua kuondoka.


Kipa huyo mwenye miaka 28 makuzi yake ya soka aliyapata kwenye chuo cha soka cha Samuel Eto'o, kwa sasa anaidakia klabu ya Nimes Olympique ya Ufaransa inayoshiriki ligi ya National, ambayo ni Ligi Daraja la Pili nchini humo.


Ahmed akizungumzia hilo pia alisema, "kwa sasa tetesi za usajili ndiyo kipindi chake, hivyo siwezi kuzuia kile kinachosemwa, lakini taarifa kamili za klabu kuhusu usajili na wachezaji tunaowaongezea mikataba na hata wale tutakaowaacha zitatolewa kwa utaratibu maalum baada ya Ligi Kuu kumalizika," alisema Ahmed.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.