Kila Mtu Ana Ubabe Wake Ligi Kuu England

 

Kila Mtu Ana Ubabe Wake Ligi Kuu England

Katika Ligi Kuu England, kwa wikiendi iliyopita, hakukuwa na purukushani za kwenye vita ya kusaka ubingwa.


Arsenal ilikuwa mapumzikoni wakati Liverpool na Manchester City ambao ni washindani kwenye mbio hizo walikuwa na majukumu mengine.


Liverpool ilikuwa na shughuli ya kuikabili Manchester United huko Old Trafford kwenye robo fainali ya Kombe la FA, wakati Man City ilikuwa na kasheshe la kuwakabili Newcastle United kwenye mechi hiyo za nane bora ya Kombe la FA, huku mechi nyingine ilishuhudia Chelsea ikicheza na Leicester City na Wolves ikikipiga na Coventry City.


Jambo hilo lilifanya ule moto wa kuwania ubingwa kwenye Ligi Kuu England kuwa kimya wikiendi iliyopita. Hata hivyo, shughuli ilikuwa kwenye kusaka Top Four, ambapo Aston Villa na Tottenham Hotspur zilikuwa mzigoni kujaribu kushushana kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo.


Spurs ilikuwa na mchezo Jumamosi wakati ilipokipiga na Fulham na ushindi kwenye mchezo huo ungewapandisha kutoka nafasi ya tano hadi ya nne katika msimamo wa ligi, wakisubiri matokeo ya Aston Villa iliyokuwa na mechi Jumapili dhidi ya West Ham United.


Kilichotokea, Spurs ilishindwa kutumia fursa na hivyo kukutana na kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Fulham. Hilo liliwaweka kwenye mashaka makubwa ya kuongeza pengo la pointi dhidi ya Aston Villa kwenye nafasi ya nne, ambao walikuwa na mechi siku inayofuata.


Hata hivyo, kikosi hicho cha Unai Emery kilishindwa kutumia nafasi baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na West Ham, hivyo kufanya pengo la pointi baina ya timu hizo mbili zinazowania nafasi kwenye Top Four kuwa tatu.


Lakini, Spurs ina mechi moja mkononi ambayo kama itashinda kwa idadi nzuri ya mabao yanayoanzia 2-0, basi itapanda hadi kwenye Top Four.


Mechi nyingine za Ligi Kuu England zilizopigwa wikiendi hii ni zile za vita ya kupambana kujinasua kwenye kasheshe la kushuka daraja.


Burnley ikiwa nyumbani iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Brentford, huku Luton Town na Nottingham Forest zilitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 na hivyo kufanya vita hiyo ya kupambana kubaki kwenye Ligi Kuu England msimu ujao kuzidi kuwa kali.


Wakati timu zikiwa kwenye mchakamchaka huo, kila moja ikisaka matokeo ya kuwafanya kuwa pazuri kwenye ligi hiyo, unawajua wenye namba za kutisha kwenye mikikimikiki hiyo kwa msimu huu?


VINARA WA MABAO Straika wa Man City, Erling Haaland ndiye anayeshika usukani kwa mastaa waliofunga mara nyingi kwenye Ligi Kuu England akiwa ametikisa nyavu mara 18 na kufuatiwa na mkali wa Aston Villa, Ollie Watkins mwenye mabao 16.


Mohamed Salah wa Liverpool yupo nafasi ya tatu na mabao yake 15, sawa na ambayo amefunga Dominic Solanke wa Bournemouth, huku tano bora ikikamilishwa na Jarron Bowen wa West Ham na Son Heung-Min wa Tottenham Hotspur, ambao kila mmoja amefunga mabao 14. Jambo hilo linafanya vita ya kusaka Kiatu cha Dhahabu kuwa matata kwelikweli kwa msimu huu.


VINARA WA ASISTI Ukiweka kando wafungaji wa mabao, kuna wale ambao wanapika mabao hayo kwa maana ya kupiga pasi za mwisho (asisti). Kwenye Ligi Kuu England kuna mastaa hao ni kiboko kwa kuasisti na kuzifanya timu zao kufanya vyema na kushika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.


Pascal GroƟ wa Brighton ndiye kinara, akiwa ameasisti mara 10, sawa na Kieran Trippier wa Newcastle United na Watkins wa Aston Villa, ambao pia wameasisti mara 10 kwenye ligi hiyo msimu huu.


Pedro Neto wa Wolves ameasisti mara tisa, sawa na Mo Salah, anayekamilisha tano bora, ambapo mkali huyo wa Liverpool, naye ameasisti mara tisa kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Tofauti na misimu mingine, ambapo viungo wamekuwa wakitamba kama kwenye eneo hili kama Bruno Fernandes na Kevin De Bruyne, msimu huu mambo yamekuwa kinyume kabisa.


VINARA WA PASI Mpira pasi wanasema, lakini kuna wachezaji hao wenyewe wanapokuwa ndani ya uwanja, wamekuwa watu wa kupiga pasi nyingi kuliko wengine. Jambo hilo ndilo linalofanya kuwapo kwa mastaa ambao wanaongoza kwa kupiga pasi na kwenye Ligi Kuu England, Rodri wa Man City, ndiye kinara wa pasi kwa msimu huu, ambapo hadi sasa amepiga pasi 2,634, akifuatiwa na Lewis Dunk wa Brighton, aliyepiga pasi 2,515.


Kwenye namba tatu, yupo William Saliba wa Arsenal mwenye pasi 2,223 na kisha Pascal GroB wa Brighton mwenye pasi 2,116, huku tano bora ikikamilishwa na Jan Paul van Hecke mwenye pasi 2,083. Orodha hiyo inatawaliwa na mastaa wa Brighton, hiyo ni ishara kwamba kikosi hicho kinapiga gonga nyingi sana..


VINARA WA CLEAN SHEET Arsenal inashika usukani wa Ligi Kuu England na hilo pengine linachangiwa kwa kiasi kikubwa na uimara wa mtu wao wa golini, kipa David Raya, ambaye ndiye anayeongoza kwa clean sheet, kwa maana ya kucheza mechi bila ya kuruhusu bao. Kipa huyo kwa msimu huu, ameshuhudia mechi tisa alizocheza bila ya wavu wake kuguswa, huku Andre Onana wa Man United akishika namba mbili, akiwa na clean sheet nane, sawa na Bernd Leno wa Fulham, Jordan Pickford wa Everton na Ederson wa Man City, ambaye anakamilisha tano bora kwa kuwa na mechi nane alizocheza bila ya kuokota mpira kwenye nyavu zake katika Ligi Kuu England.


Hiyo ina maana, vita ya Kipa Bora wa msimu kwenye Ligi Kuu England, vita yake itakuwa kali sana msimu huu kutokana na namna walivyokabana koo..


MASHUTI GOLINI Kwenye soka la kisasa, namba zinakusanywa hata kwenye orodha ya timu zilizopiga mashuti mengi yaliyolenga goli. Timu itakayocheza bila ya kuwa na shuti la kulenga goli, inahesabika kuwa imefeli na imezidiwa kwenye mchezo huo husika.


Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, wachezaji walioongoza kwa kupiga mashuti yaliyolenga goli ni straika Haaland mwenye mashuti 44, akifuatiwa na Watkins, aliyepiga mashuti 40, kisha Darwin Nunez wa Liverpool, mashuti 37, huku staa wa Man City, Phil Foden akishika namba nne kwa kupiga mashuti yaliyolenga goli mara 35, sawa na Mo Salah wa Anfield, ambaye pia amepiga idadi hiyo ya mashuti 35 golini..


KUGUSA MPIRA SANA Unahitaji kuwa na mpira muda mrefu ili kupanga mipango ya kufunga na hatimaye kushinda mechi. Lakini, kwa timu kufanya hivyo, itahitaji kuwa na aina ya wachezaji ambao watakuwa wazuri kwenye kujaribu kuwa na mpira mara nyingi ndani ya uwanja na hilo ndilo linalosababisha kuwapo na wachezaji waliogusa mpira mara nyingi uwanjani.


Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, Rodri wa Man City, ndiye aliyegusa mpira mara nyingi, 2,989, akifuatiwa na Dunk wa Brighton, aliyegusa mara 2,735, kisha GroB wa Brighton, aliyegusa mata 2,659 na namba nne ni Saliba wa Arsenal, amegusa mpira mara 2,443 na tano bora inakamilishwa na Trippier, aliyegusa mpira mara 2,360.


DAKIKA NYINGI Kwenye Ligi Kuu England kuna timu zimecheza mechi 29 na nyingine 28, lakini kwenye vikosi vya timu hizo, kuna wachezaji hao, wamejaribu kucheza kila mechi na kuwa muda mwingi ndani ya uwanja.


Kutokana na hilo, kunapatikana wachezaji waliocheza dakika nyingi na kwa msimu huu, Thomas Kaminski wa Luton, ndiye aliyecheza dakika nyingi, 2,610, hiyo ina maana amecheza kila dakika katika msimu huu, sawa na Bernd Leno wa Fulham, naye amecheza kila dakika kwenye msimu huu, dakika 2,610.


Watkins wa Aston Villa amecheza dakika 2,568, akifuatiwa na Maximilian Kilman wa Wolves, aliyecheza dakika 2,520, sawa na Emiliano Martinez wa Aston Villa, Onana wa Man United, Saliba wa Arsenal na Jordan Pickford wa Everton kwa kuwataja tu kwa uchache, ambao wamecheza dakika 2,520, sawa na mechi 28.


KADI ZA NJANO Kwenye Ligi Kuu England msimu huu kumeshuhudiwa wachezaji wakorofi pia, ambao hawapendi kupitwa uwanjani na matokeo yake yake wamekuwa akifanya madhambi mengi na kuonyeshwa kadi za njano mara nyingi.


Staa wa Fulham, Joao Palhinha, ndiye mchezaji anayeongoza kwa kadi za njano, akionyeshwa mara 12, akifuatiwa na Edson Alvarez wa West Ham United, aliyeonyesha mara 10, huku Bruno Guimaraes wa Newcastle United akionyeshwa kadi tisa za njano sawa na Nicolas Jackson wa Chelsea, ambapo straika huyo ameonyesha kadi tisa za njano.


Baada ya hapo kuna kundi la mastaa walionyeshwa kadi za njano mara nane, ambao ni Jayden Bogle wa Sheffield United, Bruno Fernandes wa Man United, Nelson Semedo wa Wolves, Moises Caicedo wa Chelsea na Anthony Gordon wa Newcastle United.


KUMWAGA MAJI Mchakamchaka wa Ligi Kuu England msimu huu umeshuhudia mastaa wa maana wakionyesha umahiri wao kwenye kupiga krosi ili kusaidia timu zao kufanya mashambulizi na hatimaye kufunga mabao.


Alfie Doughty wa Luton, ndiye anayeongoza kwa kupiga krosi kwenye Ligi Kuu England msimu huu, akipiga krosi 257, akifuatiwa na Trippier wa Newcastle, aliyepiga krosi 204, huku GroB wa Brighton akipiga krosi 173, Fernandes krosi 170, Dwight McNeil wa Everton amepiga krosi 160, wakati Andreas Pareira wa Fulham amepiga krosi 159 na kuonyesha umahiri wa wamwaga maji kwenye Ligi Kuu England msimu huu..


NAMBA NYINGINE Kila mtu na makali yake, ambapo Elijah Adebayo wa Luton amefunga mara nyingi kwa kichwa, mabao manne, sawa na Jarrod Bowen wa West Ham, Gabriel wa Arsenal, Scott McTominay wa Man United na Chris Wood wa Nottingham Forest, huku Nunez wa Liverpool akiongoza kwa kugongesha nguzo, mara tisa, akifuatiwa na Watkins mara nne, wakati waliongoza kwa kuotea ni Nunes, mara 25, Jackson wa Chelsea mara 23, Bowen mara 20, Anthony Elanga wa Nottingham Forest mara 18.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.