Chama Atoa Siri ya Kuwaadhibu Mashujaa

Chama Atoa Siri ya Kuwaadhibu Mashujaa


Mfungaji wa mabao mawili ya ushindi ya Simba SC, Kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chota Chama amesema maelekezo yaliyotolewa na Kocha Mkuu Abdelhak Benchikha wakati wa mapumziko, yalikuwa chachu ya kuibuka na ushindi dhidi ya Mashujaa FC.


Simba SC ilichomoza na ushindi huo jana Ijumaa (Machi 15), katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam, na kufanikiwa kufikisha alama 44 zinazoiweka nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu.


Chama amesema walikosa utulivu walipofika katika lango la mpinznai wao katika kipindi cha kwanza, lakini kipindi cha pili walikuwa makini kwa kufuata maelekezo ya Kocha wao Benchikha na kupata ushindi huo muhimu.


“Mchezo ulikuwa mzuri mgumu, hatukucheza vizuri katika kipindi cha kwanza kwa sababu hatukuwa na utulivu kwenye eneo la mwisho la wapinzani wetu, lakini kipindi cha pili kocha alitupa maelekezo na kufanya mabadiliko tulifanikiwa kupata mabao mawili ya ushindi.”


“Tulifanikiwa kutengeneza nafasi kadhaa katika kipindi cha pili na tumebahatika kupata mabao mawili, ambayo yametupa nafasi ya kuongeza alama tatu nyingine katika mpango wetu msimu huu.”


“Ninawashukuru sana mashabiki wa Simba SC kwa ushirikiano na nguvu wanazotupa, naamini kwa sasa wameanza kutuombea sana, kwa hiyo tunashukuru na tunawapenda na tunawaombea furaha ili mambo yazidi kusomba mbele.” amesema Chama

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.