TFF yaipitisha Al Hilal kucheza Ligi Kuu Bara

 

TFF yaipitisha Al Hilal kucheza Ligi Kuu Bara

Klabu maarufu ya Al Hilal ya Sudan itashiriki Ligi Kuu ya Bara msimu ujao lakini kwa vigezo maalumu, Mwanaspoti limeambiwa.


Si klabu hiyo tu, hadi waamuzi wa soka wa Sudan walioko Tanzania watachezesha Ligi msimu ujao kutokana na machafuko yanayoendelea nchini kwao yaliyosababisha michezo kusimama kwa muda usiojulikana.


Mwanaspoti linajua Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF), imeshakutana na kulipitisha suala hilo tayari kwa msimu ujao.


Cliford Mario Ndimbo, ambaye ni Ofisa Habari wa TFF, amelithibitishia Mwanaspoti kwamba Hilal itacheza kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao lakini kwa vigezo maalum lengo likiwa kuongeza ushindani na kuitangaza Ligi yetu.


"Ni kweli Hilal wameomba kushiriki Ligi yetu na suala lao limeshajadiliwa na kupitishwa na Kamati ya Utendaji, kwahiyo msimu ujao watacheza mechi zote za Ligi kama timu nyingine yoyote ya Tanzania," alisema Ndimbo.


"Tofauti yao na timu nyingine ni kwamba pointi zao hazitahesabiwa, watashiriki kama mechi za kirafiki wala kwenye msimamo hawatasomeka, TFF imewakubalia ombi lao kwavile litakuwa na faida kubwa kwenye ligi yetu.


"Hilal ni timu kubwa wataitangaza ligi yetu, watatoa ushindani wa kweli kwa timu zetu, hata mapato yataongezeka kwa klabu zetu kwavile itapata nafasi ya kucheza na timu zote tofauti na awali ambapo ilicheza dhidi ya timu za Dar es Salaam tu," aliongeza Ndimbo.


Mbali na timu hiyo, pia TFF imewapitisha waamuzi wote wa Sudan walioko Tanzania kuchezesha Ligi msimu ujao kama sehemu kuongeza ubora kwavile kwasasa wamekuwa tu nchini wakifanya mazoezi.


Uamuzi huo wa TFF, huenda ni wa kwanza wa aina yake hapa nchini katika miaka ya hivi karibuni kwa timu ngeni kucheza Ligi ya nchi nyingine ili kujiweka fiti bila kupata chochote.


Ikumbukwe Hilal ilishindwa kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa katika dakika za mwisho msimu huu na tayari imetuma ofa kwa klabu ya Azam ikitaka kumsajili straika wao, Prince Dube kama ilivyo kwa Simba.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.