Kocha Robertinho Aipa Mbinu Young Africans
Wakati kikosi cha Young Africans kikiendelea na maandalizi ya mchezo wa mzunguuko wa pili wa Kundi D, Ligi Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Kikosi cha Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameibuka na kuwapa mbinu Wananchi za kuwakabilia wababe hao wa soka Barani Afrika.
Robertinho, aliilazimisha Al Ahly sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Michuano ya Africans Football League uliopigwa jijini Dar es salaam, kisha kwenda kutoka nao sare ya bao 1-1 jijini Cairo na kutolewa hatua ya Robo Fainali kwa faida ya mabao ya ugenini kabla ya kufurushwa na mabosi wa Msimbazi baada ya kipigo cha mabao 5-1 kilichotolewa na Young Africans, Jumapili ya Novemba 6.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil, ambaye kwa sasa yupo Saudi Arabia kwa ajili ya mapumziko amesema Young Africans kama wanataka kushinda mchezo huo lazima wajipange kwa kutumia mifumo miwili kwa wakati mmoja.
Robertinho amesema Young Africans inavweza kuimaliza Al Ahly kwa Kutumia mfumo wa 4-2-3-1 wakati wakiwa hawana mpira lakini watakapokuwa wanashambulia wanaweza kubadilika na kutumia 4-3-3 ili kurahisisha mashambulizi.
Pia amewaongezea madini kuwa, Ahly nao hubadilika wanapokuwa hawana mpira wakitumia mfumo wa 4-2-3-1 lakini wakiwa wanashambulia hutumia ule wa 4-4-2.
“Al Ahly wanacheza tofauti wanapokuwa nyumbani na ugenini kwa kuwa Yanga itaanzia nyumbani, ndio wanatakiwa kuucheza huu mchezo kwa kuhitaji matokeo mazuri lakini wanatakiwa kuwa makini kwa kuwa wapinzani wao wanapenda sana kucheza soka la kushambulia,” amesema Robertinho.
“Kama Young Africans watatumia mfumo wa 4-3-3 wakati wa kushambulia utawafanya kuwa na idadi nzuri kule mbele katika mashambulizi yao ambayo itawapa wakati mgumu mabeki wa Al Ahly ambao hawana utulivu sana.
“Ahly hawana kasi sana ya kukimbia kurudi nyuma kujilinda hili lazima Young Africans wanatakiwa kulitumia kwa kucheza mpira wa kasi ili wafike langoni kwao kuwapa presha mabeki wao.
Pia, Robertinho amesema Young Africans ina wachezaji watatu wenye ubora, Stephanie Aziz KI, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli kama wakiamka vizuri siku ya mchezo wanaweza kuwa hatari mbele ya Ahly, wakati timu yao ikiwa na mpira kutokana na ubora wao wa kujua kukimbia haraka.
“Young Africans ina watu wanaojua kukimbia na mpira Aziz Ki, yule aliyetufunga mabao mawili (Maxi) na yule mwenye nywele nyeupe (Pacome) ni wachezaji wazuri wenye kasi kulekekea lango la mpizani kama watakuwa vizuri siku ya mchezo wanatakiwa kuipa “wakati mgumu Ahly”
“Kama wakiona mchezo unakuwa ngumu wasisite kubadilika na kutumia washambuliaji wawili kule mbele ili kuzidi kuwapa presha mabeki wa Ahly ni wazuri lakini wanapitika.”
Young Africans itavaana na Al Ahly ikiwa wiki moja tangu inyukwe mabao 3-0 na CR Belouizdad ya Algeria katika mchezo wa Kundi D, huku wageni wao wakitoka kushinda idadi kama hiyo dhidi ya Medeama ya Ghana.