Baaada ya mwalimu kufanya Rotation timu imetoka kwenye kufunga goli moja dhidi ya Medeama hadi magoli manne hii leo dhidi ya Mtibwa , Je mpinzani dhaifu au mfumo umelipa ____?
YANGA imefanikiwa kushinda mchezo wake wa tisa kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, huku Aziz Ki akiendelea kutakata.
Yanga ikiwa kwenye Uwanja wa Azam Chamazi sehemu ambayo haijapoteza mchezo wa ligi msimu huu, imeichapa Mtibwa Sugar mabao 4-1, mawili yakiwekwa kimiani na Aziz Ki ambaye amefikisha mabao tisa kwenye ligi kwa sasa.
Ki alifunga bao la kwanza kwenye mchezo huo kwa mkwaju wa penalti dakika ya 45 kipindi cha kwanza, huku akifunga lingine dakika ya 66, baada ya kuwatoka mabeki wawili wa Mtibwa na kumfunga kirahisi kipa Mohamed Makaka akipokea pasi ya Kibwana Shomari.
Yanga ambayo imekuwa bora kwenye kupachika mabao msimu huu, ilifunga bao lake la tatu kupitia kwa Kennedy Musonda kwa shuti kali katika dakika ya 76, likionekana kuwa bao la kuvutia hadi dakika hiyo, lakini Skudu Makudubela akamlipa kwa kufunga bao safi ambaye naye alilipwa na Seif Karihe ambaye alifanya ubao usomeke 4-1.
Yanga mwendo wa mabao
Huu ulikuwa mchezo wa kumi kwa Yanga kwenye Ligi Kuu Bara, lakini timu hiyo ikiwa inaonyesha kiwango cha juu kwenye michezo yake yote.
Yanga ikiwa nyuma kwa michezo miwili, tayari washambuliaji wake wameshafunga mabao 30 kwenye ligi hiyo ikiwa nyuma ya Azam ambao wanaongoza kwa tofauti ya pointi moja tu.
Hata hivyo, timu hiyo inaendelea kuonyesha ubora kwenye safu ya ulinzi ikiwa imeruhusu mabao sita ambayo ni machache kuliko timu zote kwenye ligi kuu hadi sasa.
Aziz Ki hakamatiki
Mabao mawili yaliyofungwa na Aziz Ki yanamfanya kuwa kinara kwenye chati akiwa na mabao tisa, mawili mbele ya Maxi Nzegeli, Feisal Salum na Jean Baleke ambao kila mmoja amefunga mara saba.
"Namuona Aziz Ki kila siku anabadilika, naamini huko mbele atakuwa bora zaidi alisema kocha wa Yanga Miguel Gamondi"
Shekhan atambulishwa
Wakati timu zikiwa mapumziko mashabiki wa Yanga waliokuwa uwanjani wakapata fursa ya kutambulishwa mchezaji mpya wa timu hiyo Shekhan Khamis aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea JKU akiletwa uwanjani hapo na makamu wa Rais wa timu hiyo Arafat Haji.
Mara baada ya kuingia uwanjani Shekhan alizunguka Uwanja mzima na kuwasalimia mashabiki wa Yanga kisha kutoka na kwenda jukwaani huku mashabiki wakimshangilia kila alipopita.