Simba Watatoboa Kweli...

 

Simba Watatoboa Kweli...

Simba itaanza harakati zake za kuwania kuingia katika nafasi iliyozoea ya robo fainali kesho licha ya kwamba ubora wa kikosi hicho kwa siku za karibuni umeonekana kuwapa shaka mashabiki wake wakijiuliza je watatoboa kweli?


Wekundu wa Msimbazi wataikaribisha Asec Mimosas ya Ivory Coast kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi utakaofanyika kesho kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.


Ndani ya miaka mitano mfululizo tangu 2019 Simba imeingia hatua ya makundi ya michuano ya CAF mara tano ukiwamo msimu huu, ikifanya hivyo mara nne kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na mara moja kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.


Ilitinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/2019, 2020/2021/ 2022/2023 na msimu huu wa 2023/2024 mbali na ile ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2020/2021


WAPINZANI WANAJUANA


Simba imepangwa kundi B pamoja na Wydad AC ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Jwaneng Galaxy ya Botswana lakini jambo zuri ni kwamba wapinzani wake wote iliwahi kucheza nao kwa vipindi tofauti.


Iliwahi kutolewa na Jwaneng Galaxy Oktoba 24, 2021 kwenye mchezo wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuchapwa mabao 3-1 nyumbani baada ya kushinda ugenini kwa mabao 2-0 (Oktoba 7) hivyo kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.


Pia iliwahi kukutana na Asec Mimomas kwenye hatua ya makundi msimu wa 2021/202, ikiwa kundi D pamoja na RS Berkane ya Morocco na USGN ya Nigeria.


Ilicheza na Asec Mimosas kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Februari 13, 2022 na Simba kushinda mabao 3-1 kabla ya kwenda kuchapwa ugenini mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika Machi 20, 2022.


Hata hivyo, katika kundi hilo, Simba na RS Berkane zilifanikiwa kufuzu robo fainali.


Wekundu wa Msimbazi pia wanaifahamu vema Wydad AC kwani ndio iliyowatoa kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita kwa penalti 4-3.


Simba iliifunga Wydad nyumbani kwa bao 1-0 kabla ya Wekundu wa Msimbazi kulala kwa matokeo kama hayo ugenini hivyo mchezo huo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti na wapinzani wao kuibuka wababe.


Wydad AC walifika hadi fainali katika michuano hiyo ambapo walikutana na Al Ahly, wakitoka sare ya bao 1-1 nyumbani na kisha kuchapwa mabao 2-1 ugenini hivyo Al Ahly kuwa mabingwa.


KIWANGO CHAWAPA HOFU MASHABIKI


Kiwango ambacho Simba ilikionyesha tangu mechi ya hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya Power Dynamos ya Zambia kinawapa wasiwasi mashabiki wa klabu hiyo ambao wanajiuliza je timu yao kweli itaendeleza ilipoishia msimu uliopita?


Simba ilitoka sare ya 2-2 ugenini dhidi ya Power Dynamos kisha ikatoka sare ya 1-1 nyumbani na kufuzu hatua ya makundi kwa kutumia kanuni ya faida ya mabao ya ugenini.


Hata hivyo, mashabiki wa klabu hiyo wanatakiwa kuendelea kuiunga mkono timu yao kwani imekuwa ikifanya maajabu mara nyingi kwenye michuano ya kimataifa na tangu ifuzu hatua ya makundi kwa miaka mitano ya karibuni imekuwa ikitinga robo fainali.


IKIINGIA MAKUNDI TU BASI ROBO HII HAPA


Unaambiwa hii ndio Simba ya kimataifa buana kwani tangu mwaka 2019 imekuwa na rekodi nzuri ya kuvuka hatua ya makundi na kutinga robo fainali katika michunao hiyo ya CAF.


Kila Simba ilipoingia hatua ya makundi ndani ya misimu minne mfululizo basi ilitinga robo fainali hivyo kuonyesha kuwa ni wababe katika eneo hilo.


Katika miaka mitano sasa, Simba imeingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu na mara moja kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na mara zote hizo imetoboa na kutinga robo fainali hivyo watu wanasubiri kuona je msimu huu wataendelea walipoishia?


2018/2019


Katika msimu huu Simba iliingia hatua ya makundi pamoja na timu za Al Ahly ya Misri, AS Vita ya Congo na JS Saoura ya Algeria.


Ilimaliza nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na pointi tisa nyuma ya Al Ahly iliyokuwa na pointi 10 hivyo timu zote mbili kufuzu hatua ya robo fainali.


Katika hatua ya makundi Simba ilishinda mechi zote tatu za nyumbani kwa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura, iliichapa Al Ahly bao 1-0 na kuifunga AS Vita mabao 2-1 lakini ilipoteza mechi zote tatu za ugenini kwa mabao 5-0 dhidi ya Al Ahly na AS Vita na ilifungwa na JS Saoura mabao 2-0.


Baada ya kutinga robo fainali Simba ikatolewa na TP Mazembe ya Congo baada ya kutoka suluhu nyumbani na kuchapwa mabao 4-1 ugenini.


2020/2021


Msimu huu pia Simba ilifanya vizuri zaidi kwenye hatua hii ya makundi ikimaliza kinara wa kundi A kwa kukusanya pointi 13 ikifuatiwa na Al Ahly ya Misri iliyomaliza ya pili kwa pointi 11 na zote mbili kutinga robo fainali huku AS Vita ikiwa ya tatu baada ya kuvuna pointi saba na Al Merrikh ya Sudan ikishika mkia baada ya kuambulia pointi mbili.


Simba ilikusanya alama hizo kwa kushinda mechi zote tatu za nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly kisha ikainyuka Al Merrikh mabao 3-0 na kuitandika AS Vita mabao 4-1. Pia ilishinda ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya AS Vita na kufungwa bao 1-0 na Al Ahly.


Msimu huu, Simba ilitolewa hatua ya robo fainali na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini baada ya kufungwa ugenini mabao 4-0 licha ya kwamba ilishinda nyumbani kwa mabao 3-0.


2021/22


Huu ndio msimu pekee ambao Simba ilishindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ndani ya miaka hii mitano tangu 2019 lakini ikafuzu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.


Simba ilitolewa raundi ya pili na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa kufungwa mabao 3-1 nyumbani licha ya kushinda ugenini kwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza.


Baada ya Simba kushindwa kufuzu makundi, Simba ikaangukia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambako iliifunga Red Arrows ya Nigeria mabao 3-0 nyumbani na kuchapwa mabao 2-1 ugenini. Hata hivyo, ikafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.


Katika michezo ya makundi Simba ilitakata na kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi D ikiwa na pointi 10 sawa na vinara RS Berkane ya Morocco wakati Asec Mimosas ilishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tisa wakati USGN ya Nigeria ilimaliza mkiani kwa pointi tano.


Simba na RS Berkane zikafuzu robo fainali ya michuano hiyo kutoka kundi hilo lakini Wekundu wa Msimbazi wakashindwa kwenda nusu fainali baada ya kufungwa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa penalti 4-3 baada ya timu hizo kila moja kushinda nyumbani kwa bao 1-0.


2022/2023


Simba iliendelea kutakata kwenye hatua ya makundi hata katika msimu huu baada ya kumaliza nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa nyuma ya Raja Casablanca ya Morocco iliyomaliza ikiwa kinara wa kundi C baada ya kuvuna pointi 16. Horoya ya Guinea ilimaliza ya tatu ikiwa na pointi saba wakati Vipers ya Uganda ilishika mkia ikiwa na pointi mbili.


Raja Casablanca na Simba zikafuzu kucheza robo fainali lakini Wekundu wa Msimbazi wakatolewa katika hatua hiyo kwa kufungwa na Wydad AC kwa penalti 4-3 baada ya timu hizo kufungana bao 1-0 kila mmoja kwenye uwanja wa nyumbani.


KWA MKAPA HATOKI MTU


Asikwambie mtu Simba huwa anakuwa mnyama mkali sana hasa anapocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Benjamini Mkapa kwani rekodi zinaonyesha tangu 2019 timu hiyo imepoteza mchezo mmoja tu kati ya 12 ambayo imecheza kwenye hatua ya makundi ya michuano ya CAF.


Mchezo huo ambao Simba ilipoteza ni dhidi ya Raja Casablanca uliofanyika Februari 18 mwaka huu baada ya kuchapwa mabao 3-0.


Mechi nyingine 11 Simba ilishinda hivyo kuonyesha kuwa rekodi zinaibeba kufanya vizuri hata kwenye michuano ya msimu huu.


Ukiondoa michezo hiyo 12 ya hatua ya makundi pia Simba ilishinda michezo mitatu kati ya minne iliyocheza nyumbani kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF. Mchezo mmoja tu kwenye hatua hiyo ilitoka suluhu dhidi ya TP Mazembe Aprili 6, 2019.


Ilishinda kwa mabao 3-0 dhidi ya Kaizer Chiefs Aprili 22, 2021, ikaifunga Orlando Pirates kwa bao 1-0 Aprili 17, 2022 na ikaichapa Wydad Casablanca kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Aprili 22 mwaka huu

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad