Nondo tano za CAF, Wasifia Soka la Tanzania Kukua Kwa Kasi Kubwa

 

Nondo tano za CAF, Wasifia Soka la Tanzania Kukua Kwa Kasi Kubwa

Jana Dar es Salaam iligeuka kuwa jiji la soka ambapo kila kona habari kubwa ilikuwa ni juu ya uzinduzi wa mashindano mapya ya African Football League yaliyoambatana na mechi ya kwanza kati ya Simba na Al Ahly kutoka Misri.


Ukiachana na mechi, maandalizi yalivyokuwa mwanzo hadi mwisho na sherehe nzima, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe alitoa nondo tano anazoamini zitasaidia kukuza na kuboresha soka la Afrika, huku akiisifia Tanzania kutokana na soka lake kukua kwa kasi kubwa.


Motsepe ambaye ni raia wa Afrika Kusini wakati wa uzinduzi wa kombe hilo kwenye mkutano na waandishi wa habari, alisema ndoto yake ni kuhakikisha soka la Afrika linakua kama ilivyo Ulaya na kushindana kwa ukubwa zaidi.


SOKA LA VIJANA


Motsepe alisema ili soka la Afrika liendelee unahitajika uwekezaji wa tija katika soka la vijana ambako ndiko ulipo msingi wa mastaa.


“Nimezunguka sehemu mbalimbali kila unapoona maendeleo kwenye mchezo wowote jua uwekezaji wa vijana ulikuwa mkubwa.


“Nimekwenda Marekani na kufuatilia mchezo wa kikapu ambao ndio maarufu zaidi kule. Mzizi wa mafanikio yote ni vijana. Vivyo hivyo kwa timu nyingi za soka duniani,” alisema.


“Kila kiongozi wa shirikisho la soka Afrika nimemwambia nahitaji tuwekeze zaidi katika vijana na baada ya hapo tutapata matokeo chanya na kufikia malengo.”


FEDHA


Katika suala la pesa, Motsepe alikazia msumari na kusisitiza kwamba, ili soka la Afrika lipige hatua ni lazima kuwepo na uwekezaji wa kutosha na mzunguko wa pesa uwe mkubwa katika sekta hiyo.


“Tunataka wachezaji wetu wajivunie kucheza Afrika. Hawawezi kufanya hivyo kama hawalipwi vizuri. Ili walipwe vyema tunahitaji kuwa na klabu zenye nguvu ya kifedha nyingi,” alisema.


“Hapa ndipo wadhamini wanaingia. Ifike mahali Afrika tulipe wachezaji kama ilivyo kwa wenzetu. Tuweze kushindana kwenye usajili. Klabu zetu zinunue mchezaji popote pale na acheze Afrika. Hivyo klabu, wadau na kila mhusika tujitahidi kutafuta namna ya kuzipa klabu zetu mapato ili tuweze kufikia lengo hili. Tumeandaa mashindano haya.”


WAAMUZI


Akizungumzia ishu ya waamuzi, rais huyo wa CAF alisema: “Hili ni eneo lingine nyeti. Nashukuru leo tupo na miongoni mwa waamuzi bora waliotokea Pierluigi Collina atatupa uzoefu.”


“Hata hivyo, shida hii tumeibaini muda sasa. Tunaendelea kupunguza makosa hayo na njia mojawapo tunayotumia ni kutoa mafunzo sahihi.


“Hili ni eneo ambalo kila siku tunatoa mafunzo. Tunataka ifike siku waamuzi wetu wa Afrika waache kulalamikiwa lakini pia wachezeshe kwenye ngazi za juu zaidi.


“Tumekuwa tukitoa elimu kila uchao kupitia mashirikisho na tutaendelea hivyo tukiamini ipo siku hili halitakuwa tatizo tena.”


USHINDANI


Motsepe alizungumzia pia ushindani wa timu akisema kwa sasa katika ngazi ya klabu hatua imepigwa, lakini pia kwa timu za taifa akiitaja Morocco iliyofanya vizuri katika Kombe la Dunia lililopita ikiishia nusu fainali.


“Naendelea kusisitiza ushindani. Dunia ya mpira iko wazi kwa kila timu. Tuweke mikakati ya kutengenexa timu zenye ushindani, mfano TP Mazembe iliwahi kufanya vizuri kwenye mashindano ya dunia kwa klabu, sasa ile kasi ndio tunataka.


“Vivyo hivyo kwa timu za taifa tuliiona Morocco ilichofanya msimu uliopita katika Kombe la Dunia. Tunataka huo uwe mwwendelezo na kwa timu nyingine.”


USAWA NA UWAZI


Akizungumzia masuala ya uwajibikaji, usawa na uwazi, alisema: “Ni kweli hii nayo ni shida. Zipo (tuhuma) tunazozibaini na kuzifanyia kazi lakini nyingine inakuwa ngumu. Tuna mkakati wa kushawishi usawa, uwazi na uwajibikaji na tunafanyia kazi.


“Kuna baadhi ya mambo yanatokea ambayo sio sawa lakini kutokana na kutokuwa na uwajibikaji kwa baadhi ya watu yanapita. Ili tusonge mbele tunahitaji kuwa na usawa, uwazi na uwajibikaji kwenye kila tunachofanya.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.