Kylian Mbappe anaamini kuwa anastahili kuwa mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or kwa mwaka 2023 baada ya kuonyesha kiwango bora sana akizitumikia klabu ya PSG pamoja na Timu ya Taifa ya Ufaransa.
Akijibu kwenye mahojiano na TF1 swali lililouliza kama anafaa kuwa mshindi wa kinyang'anyiro cha kutwaa tuzo ya mchezaji bora zaidi duniani, Mbappe alisema.
“Ballon d'Or? Siku zote ni vigumu kuzungumzia tuzo binafsi, kwa sababu itakubidi ujipatie kipaumbele. Ni jambo ambalo si lazima ukubaliane na umma kwa ujumla.
“Je, ninastahili kushinda Ballon d'Or? Kwa vigezo vipya, kipi ni muhimu? Kuvutia watazamaji, kufunga mabao na kuchangia matokeo? Nadhani ninakidhi vigezo vyote. Nitasema ndiyo, lakini watu ndio hupiga kura na nina matumaini wakati wote.”
Ndoto za Kylian Mbappe kutwaa taji la Kombe la Dunia kwa mara ya pili mwaka 2022 ziliyeyuka baada ya kuwashuhudia Argentina ikiongozwa Lionel Messi kutwaa taji hilo. Pia Mbappe hakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Ulaya na hivyo mshambuliaji huyo atakutana na ushindani mkubwa kutoka kwa Lionel Messi pamoja Erling Haaland aliyefanikiwa kushinda makombe matatu (Treble) akiwa na Manchester City.
Na @Kubebekajr