Timu ya Polisi Tanzania imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mabao ya Polisi Tanzania yamefungwa na Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dakika ya 22, Chilo Mkama dakika ya 40 na Kelvin Sabato dakika ya 65, wakati la Mtibwa Sugar limefungwa na Nassor Kiziwa dakika ya 27.
Kwa ushindi huo, Polisi Tanzania inafikisha pointi 25, ingawa nafasi ya 15 ikizidiwa pointi nne na Mtibwa Sugar baada ya wote kucheza mechi 28.
Kuelekea mechi mbili za mwisho, tayari Ruvu Shooting imeteremka daraja na itaungana na timu itakayomaliza nafasi ya 15.
Timu zitakazomaliza nafasi ya 13 na 14 zitacheza mechi mbili maalum za mchujo nyumbani na ugenini na itayafungwa katika matokeo ya jumla itakwenda kumenyana na timu ya Championship kuwania kupanda.