Namna Raiola angejilamba vidole kwa mabao ya Haaland

 

Namna Raiola angejilamba vidole kwa mabao ya Haaland

Alifariki katika hospitali ya San Raffaele pale Milan mchana wa April 22 mwaka jana. Ni mwaka sasa. Mino Raiola, wakala kibonge hivi, tajiri na mzaliwa wa Italia aliyekulia Uholanzi. Ni mwaka sasa. Namna ambavyo nyakati zinakimbia. Umewahi kufikiria kama angekuwa hai?


Inaweza umeshayasahau matendo yake. Kama angekuwepo angekuwa mmoja kati ya watu ambao wanatamkwa sana katika soka pengine kuliko wachezaji wanaozubaa uwanjani. Alikuwa wakala maarufu pengine kuliko wachezaji wengi.


Mkononi alishikilia bidhaa adimu. Moja kati ya bidhaa hizi ni Erling Bruut Haaland. Umewahi kuwaza namna gani Raiola angetusumbua kama bado angekuwa hai, huku mkononi akiendelea kummiliki Haaland. Nadhani kwa sababu tusingekaa. Pasingekalika.


Bahati mbaya kwa Raiola kwanza kabisa aliukosa uhamisho wa Haaland kutoka Borussia Dortmund kwenda Manchester City. Nafahamu kwamba kampuni yake ya uwakala ndio iliyokamilisha uhamisho huu.


Lakini yeye mwenyewe alifariki Aprili, huku Haaland akifanikisha kwenda Manchester City Juni. Sijui kama Raiola alihusika vema, lakini ninachofahamu ni yeye, kama ilivyo sisi, hakufahamu vema ambacho Haaland alikuwa anakwenda kukifanya England.


Kulikuwa na wasiwasi kwamba Haaland huenda angepata wakati mgumu England. Uhamisho ni kamari. Kuna ambao unafaulu na kuna ambao unafeli. Na tuna maringo na Ligi Kuu ya England tukiamini kwamba ni ngumu. Viatu vinatembea na ubabe ni mwingi. Kuna ile kauli ambayo wanasoka wasiocheza England huwa wanaulizwa; "Unaweza kufanya hivi katika usiku wa baridi kali dhidi ya Stoke City ugenini?"


Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniapia kwamba Haaland asingeweza kuhamishia mabao yake kutoka Ujerumani kuja England. Kama vile aliokuwa anawafunga Ujerumani walikuwa wepesi. Kwamba maisha yangekuwa magumu kwake mbele ya kina Virgil Van Dijik na mabeki wengine wa shoka England.


Badala yake Haaland ameifanya Ligi Kuu ya England kuwa nyanya katika mkono wake. Ameirahisisha katika namna ambayo washambuliaji wote hatari waliocheza England wameshindwa kuirahisisha.


Ndani ya msimu wa kwanza tayari ametupia mabao 35 ya Ligi Kuu katika mechi 31 tu. Hakuna mchezaji aliyewahi kutupia mabao mengi ndani ya msimu mmoja katika Ligi Kuu ya England. Ameipita rekodi ya mabao 34 iliyokuwa inashikiliwa na Andy Cole. Kumbuka kwamba mkononi ana mechi tano. Anaweza kufikisha mabao 40 huyu.


Lakini tayari kwa msimu wote Haaland ana mabao 50. Haya mabao 50 kwa msimu ni viwango vya kina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakiwa Hispania wakati ule. Tulikuwa tunajumlisha mabao yao na yale ambayo walikuwa wamefunga La Liga tukaamini kwamba Ligi yenyewe ya Hispania ilikuwa imewasaidia kwa sababu ni nyepesi. Leo Haaland anafunga mabao kama haya kwa urahisi tu huku Ligi Kuu ya England ikiwa inamsaidia.


Kuna mtu anaweza kuwa amekaa katika kiti cha baa mahala fulani akiamini kwamba Haaland anafunga mabao haya kwa sababu anachezea Manchester City. Jiulize, ni wachezaji wangapi hatari wameichezea Manchester City katika kipindi hiki cha Pep Guardiola. Usisahau kumjumlisha na Sergio Aguero.


Pia jiulize ni washambuliaji wangapi waliocheza katika vikosi hatari vya Manchester United, Arsenal, Chelsea na Liverpool ambao walifanya mambo kama ya Haaland hasa katika msimu wa kwanza? Wengi wanasubiri kwa Haaland. Na hapa ndipo ambapo tungepata shida kwa Mino Raiola.


Yote haya Raiola anayafahamu. Na katika dunia ya sasa Raiola angejikuta ameshikilia moja kati ya bidhaa mbili adimu katika soko la soka kwa sasa. Kando ya Kylian Mbappe hakuna mtu hatari zaidi ya Haaland. Raiola angehakikisha bidhaa yake inasumbua sokoni kadri iwezekanavyo.


Alianza kusumbua soko mapema tu. Wakati Haaland anacheza Austria kulikuwa na uwezekano akaondoka pale moja kwa moja kwenda katika timu kubwa. Hakutaka hilo litokee na badala yake akaamua kumpeleka Borussia Dortmund. Alifanya hivyo kwa makusudi kwa sababu alijua Haaland ni mdogo na angeweza kumpitisha katika vituo vingi.


Timu kubwa zina tabia ya kumng'ang'ania mchezaji mdogo na wakaishi naye kwa muda mrefu. Yeye alitaka mchezaji apande madaraja taratibu kadri iwezekanavyo ili awe anajipatia kiasi kikubwa cha pesa kila anapohama kutoka klabu moja kwenda nyingi. Manchester United walimtaka Haaland lakini aliwapa masharti magumu makusudi.


Alijua kwamba kama wangepata Haaland kwa umri ule, wakati ule akiwa anatokea Austria, wangeweza kukaa naye kwa miaka 15. Hili asingekubali litokee. Ndio maana akampeleka Dortmund ili aweze kuvuna kitita fulani kule, kisha ampeleke kwingine avune kitita fulani, halafu ampeleke kwingine avute tena kitita fulani.


Bahati mbaya akiwa katika mchakato huu akafariki. Nadhani alikuwepo na alihusika kikamilifu katika mchakato wa kumpeleka Manchester City, ingawa kabla ya mchakato kumalizika akafariki. Kama angekuwa hai sasa hivi angekuwa katika mchakato wa kumhamisha kutoka City kwenda Real Madrid ili apate pesa yake nyingine ndefu ya udalali.


Wahanga wa kwanza wa kubwa wa tabia zake wangekuwa mashabiki wa Manchester City. Lazima Raiola angekuwa anatoa kauli za kuonyesha kwamba Haaland anaweza kuondoka muda wowote ule Manchester City. Hii ni mbinu ya kuhakikisha kwamba yeye mwenyewe anapata dau kubwa la uhalali.


Ungesikia tu wiki hii anasema; "Kuna ofa nyingi kubwa zipo mezani kwa ajili ya Haaland. Ana furaha kucheza City, lakini yupo tayari kupata changamoto mpya kwa klabu kubwa ambazo zitamhitaji. Kwa sasa tunatafakari ofa ambazo zipo mezani kwetu." Huyu ndiye Raiola ninayemfahamu. Alikuwa kivuruge hasa.


Wiki ijayo angesema; "Hakuna mchezaji mkubwa ambaye asingependa kucheza Real Madrid na Haaland ni mchezaji mkubwa ambaye Real Madrid imeonyesha juhudi za kumnyakua. Tutaongea na City kujua wanachofikiria kuhusu Haaland kwa sasa, lakini kwetu milango ipo wazi kwa Haaland kucheza popote anapojisikia."


Huyu ndiye Raiola halisi. Waulize mashabiki wa Manchester United watakwambia jinsi alivyokuwa anawasumbua kuhusu Paul Pogba wakati ule akiwa anavaa jezi yao. Waliishia kumchukia Raiola na kisha wakamchukia Pogba mwenyewe. Raiola alihakikisha Pogba hasaini mkataba mpya United na anaondoka bure. Kila siku alikuwa anamnadi kwingineko.


Na sasa angekuwa na bidhaa kama Haaland sokoni nadhani angetamba haswa. Lazima angehakikisha ama Haaland anakwenda Real Madrid au yeye anapata dau kubwa la pesa kwa Haaland kuendelea kubakia Etihad. Bahati mbaya angefariki. Kama angekuwa hai lazima uhamisho wa Haaland kwenda kwingineko ungempatia Pauni 30 Milioni yeye binafsi kama dalali.


Bahati mbaya wakati mwingine maisha hayakupi kila unachokitamani. Yanakunyima fursa ambayo wewe ulikuwa unaitamani, lakini sisi mashuhuda wengine tungetamani kuona namna ambavyo ungeitumia. Apumzike kwa amani Mino 'The Super Agent' Raiola.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.