Kocha Morocco Asikilize Hoja, TAIFA Stars Ina Tatizo la Mbinu

Kocha Morocco Asikilize Hoja, TAIFA Stars Ina Tatizo la Mbinu


Bado timu yetu inaonekana haina fomula ya kupata mabao. Inaonekana inahangaika na mwisho ni juhudi za wachezaji binafsi zinazoipa timu ushindi. Hili ni tatizo la kimbinu ambalo linaweza kutatuliwa na kocha na benchi lake la ufundi.


Hili ndilo husababisha kocha kusifiwa au kukosolewa na hili ndilo linalojenga taswira ya kocha. Kwamba anapenda kutumia aina fulani ya mchezo kwenye mazingira magumu au mepesi, anapenda wachezaji wa aina fulani kwa kuangalia fomesheni yake au anapenda mchezo wa kasi au umiliki mkubwa wa mpira ndiyo maana huteua wachezaji wa aina fulani.


Hatuoni vitu hivyo kwa Hemed Suleiman ‘Morocco’. Huwa tunaona matokeo mwishoni mwa mchezo bila ya kujua yalikujaje. Hivyo mashabiki wanapopiga kelele mchezaji kama Kelvin John ajumuishwe, lakini hajumuishwi, hawaelewi kwa nini kocha anamuacha kwa kuwa hawajui aina ya mchezo anayotumia na aina ya washambuliaji anaowataka.


Watu wanapopiga kelele Offen Chikola au Yahya Zayd wajumuishwe, hawaelewi sababu za kocha kugomea. Baada ya fainali za CHAN, Morocco alisema Kelvin anatakiwa apandishe kiwango chake. Hajamzungumzia Chikola wala Zayd, viungo wawili wa kushambulia na kuzuia wanaoonekana kupanda chati kwa kasi.


Lakini timu inapowekwa katika mazingira magumu, huoni kama benchi lina wachezaji wazuri zaidi ya waliomo uwanjani.. Wakati timu ikiwa nyuma kwa bao 1-0, Morocco alifanya mabadiliko ya mabeki wawili wa pembeni, akiwaingiza Tshabalala na Lusajo Mwaikenda. Unajiuliza timu ilikuwa inatafuta nini? Kwa maana nyingine, ukiacha Mwalimu, bado hakukuwa na chaguo bora la kuweza kushika nafasi ya Mzize au Mudathir walioonekana kutokuwa na siku nzuri.


Kwa maneno mengine, pengine Kelvin na Zayd wangeweza kusaidia. Mabadiliko ya kimbinu yangeweza kutatua tatizo la Mudathir na Mzize na timu kupata uhai iliouhitaji kupata pointi tatu muhimu ugenini.


Morocco aliwahi kusema alimuacha beki wa Yanga, Dickson Job kwa kukataa kucheza kama beki wa kulia na kwa kimo chake hawezi kucheza beki wa kati. Maneno hayo hawezi kuyarudia leo kwa mchezaji huyo ambaye ndiye nahodha wake na mwenye uhakika wa nafasi katika kikosi hicho.


Angetile Osiah

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad