Kiungo wa Timu ya Young Africans Pacome Zouzoua amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Juni wa Ligi kuu ya NBC msimu wa mwaka 2024/25 huku Miloud Hamdi aliyekuwa Yanga akichaguliwa kuwa Kocha bora wa mwezi huo.
"Pacome alionesha kiwango kizuri chenye muendelezo, akiwashinda Clatous Chama wa Yanga na Kibu Denis wa Simba alioingia nao fainali katika mchakato wa tuzo hizo za mwezi uliofanywa na Kamati ya tuzo za shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF" imesema taarifa ya Idara ya habari na Mawasiliano, Bodi ya ligi kuu Tanzania.
Kulingana na Bodi hiyo, Mchezaji Pacome alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo mitatu ambayo Yanga ilicheza mwezi huo, akifunga mabao matatu na kuhusika na bao moja kwa dakika 242 alizocheza.
Kwa upande wa Hamdi aliyeingia fainali na Taoussi wa Azam Fc na Fred Felix wa Pamba Jiji aliiongoza Yanga kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi huo na kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya NBC kwa msimu wa 2024/25. Yanga ilizifunga Tanzania Prisons 0-5, Dodoma Jiji 5-0 na Simba 2-0.
Pia kamati hiyo ya Tuzo imemchagua Meneja wa uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara Bw. Jackson Mwendwa kuwa Meneja bora wa Uwanja kwa mwezi Juni kutokana na kufanya vizuri katika Menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.