LEO turejee kile ambacho tumekuwa tukikisema tangu kuanzishwa kwa kanuni ya mtoano kuamua timu za kupanda na kushuka daraja kuanzia First League, Championship hadi Ligi Kuu. Tunasema mechi hizo hazina mizania sawa kwa timu shiriki na ipo haja ya kubadilishwa na kutumika kama zamani kwa timu zinazomaliza nafasi tatu za mwisho za kila ligi zishuke moja kwa moja badala ya kushuma mbili kisha nyingine moja kutafutwa kwa mtoano.
Hata kama ni kweli tumeiga mfumo kutoka Ujerumani. Tunadhani ingefaa kama bado tunataka mtindo wa mtoano utumike tuige ule unaotumika England ambao timu nne zinazomaliza nyuma ya bingwa wa Ligi ya Championship (EFL) na mshindi wa pili zinazopanda moja kwa moja kwenda Ligi Kuu England (EPL) zicheze zenyewe ligi ndogo kuamua moja ya kuungana na waliotangulia kupanda daraja.
Huku timu tatu za mwisho EPL zinashuka moja kwa moja na kutoa nafasi kwa zile za Championship kuwa na uhakika wa kupanda kuliko mfumo wa Kijerumani ambao mara zote umekuwa ukizibeba za Ligi Kuu kwa utimamu na hata kiuchumi. Tunalisema hili kwa kurejea kumbukumbu za mfumo wetu kuzikwamisha timu za Championship kupanda kwa utaratibu wa kucheza dhidi ya timu za madaraja tofauti na zinayocheza.