WAKATI Yanga ikiwafuatilia kwa ukaribu nyota wanne walioachwa na Simba Queens, Wekundu wa Msimbazi wamemalizana na beki wa pembeni wa Wananchi hao, Asha Omary.
Yanga iko kwenye mpango wa kuwasajili Precious Christopher na Wincate Kaari ambao wote wawili waliitumikia Yanga Princess msimu uliopita kabla ya kujiunga na Mnyama, pamoja na Asha Djafar na Riticia Nabbosa.
Akizungumza na Mwanaspoti, wakala wa mchezaji huyo, Amoc Mlandali, alisema beki huyo amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba Queens msimu ujao.
“Ni kweli amesaini mkataba wa miaka miwili Simba akitokea Yanga. Ofa ilikuwa nzuri, kwa sababu pia JKT tulikuwa na mazungumzo nao lakini hawakufikia dau tulilolihitaji na mchezaji mwenyewe hakutaka kusaini,” alisema Mlandali.
Asha kwa sasa yuko nchini Morocco na kikosi cha Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, kwenye mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON).
Kwenye mashindano hayo ambayo Stars ilipangwa Kundi C, Asha alicheza mechi zote mbili dhidi ya Mali ambapo Tanzania ilipoteza kwa bao 1-0, na dhidi ya Afrika Kusini ilipotoka sare ya 1-1.
Hii si mara ya kwanza kwa beki huyo chipukizi kuitwa na kucheza kwenye kikosi cha Stars.
Chini ya kocha Bakari Shime, chipukkizi huyu alicheza pia mashindano ya CECAFA Senior Women Championship yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi.