Aziz Ki, ameibua gumzo kubwa mitandaoni baada ya kubadilisha picha ya wasifu katika akaunti yake ya Instagram.
Hapo awali, Aziz Ki alikuwa ameiweka picha yake akiwa amevaa jezi ya Klabu ya Yanga SC ya Tanzania, lakini sasa ameibadilisha na kuweka picha mpya inayomuonesha akiwa amevalia jezi ya Wydad Casablanca ya Morocco.
Hatua hii imezua maswali mengi na hisia tofauti miongoni mwa mashabiki wa soka, hasa wale wa Yanga, ambao wamekuwa wakimkumbuka mchezaji huyo kwa mchango wake mkubwa ndani ya klabu hiyo.
Mabadiliko haya yamekuja katika kipindi ambacho tayari kuna tetesi zinazozagaa kuhusu hatma ya Aziz Ki ndani ya Wydad Casablanca.
Licha ya kusajiliwa kwa mbwembwe kubwa kutoka Yanga SC na matarajio makubwa, nyota huyo hakupata nafasi ya kutosha ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Wydad, hali iliyozua maswali kuhusu mustakabali wake.
Baadhi ya wachambuzi wa soka na mashabiki wameanza kuamini kuwa huenda kiungo huyo akarejea Yanga SC, hasa kutokana na taarifa kuwa mkataba wake una kipengele kinachomruhusu kufanya hivyo endapo hatapata nafasi ya kucheza ya kutosha.
Aziz Ki alipojiunga na Yanga, alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na kiwango chake kizuri uwanjani, na alikuwa miongoni mwa wachezaji waliopendwa zaidi na mashabiki wa timu hiyo.
Uwepo wake ulichangia mafanikio kadhaa ya klabu hiyo, ikiwa ni pamoja na kutwaa mataji ya ndani na kushiriki michuano ya kimataifa kwa mafanikio.
Hali hiyo inawafanya mashabiki wa Yanga kuendelea kumtamani arejee, wakiamini bado anaweza kuwa msaada mkubwa kwa kikosi chao.
Kwa sasa, bado hakuna taarifa rasmi kutoka kwa Aziz Ki wala klabu yake ya sasa kuhusu mustakabali wake, lakini mabadiliko ya picha ya wasifu kwenye Instagram yameongeza mvutano na mijadala mitandaoni
. Wengi wanaona huenda ni ishara ya mabadiliko yanayokuja, huku baadhi wakihisi huenda ni njia ya mchezaji huyo kuwasilisha ujumbe kwa mashabiki na klabu yake ya zamani.
Hata hivyo, mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona kama kweli atarejea Yanga au ataendelea kupambana kutafuta nafasi ndani ya kikosi cha Wydad Casablanca.