Kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Hemed Morocco, ameweka wazi azma yake ya kuibuka na ushindi dhidi ya DR Congo katika mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2025, utakaopigwa leo, Alhamisi Oktoba 10, 2024.
Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari leo, Morocco amesisitiza kuwa Taifa Stars inahitaji alama tatu muhimu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu michuano hiyo mikubwa barani Afrika, ambayo itafanyika nchini Morocco.
"Ni mechi muhimu sana kwetu. Tumefanya maandalizi mazuri na kikosi kimejaa wachezaji wenye uzoefu wa mashindano makubwa," alisema Morocco kwa kujiamini.
Kocha huyo pia ametangaza kuwa straika hatari, Mbwana Samatta, ataungana na kikosi kwa ajili ya mchezo huo.
"Tuna furaha kumkaribisha Samatta, ambaye ameonyesha kiwango bora sana kwenye klabu yake. Uwepo wake utaongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji, na naamini tutafanikiwa kuchukua alama tatu, japokuwa tunatambua kwamba hautakuwa mchezo mwepesi," aliongeza.
Mchezo huu ni sehemu ya kampeni ya Taifa Stars ya kutafuta nafasi kwenye michuano ya AFCON 2025, ambapo Tanzania inahitaji matokeo mazuri ili kuhakikisha inafuzu kwenye mashindano hayo yatakayofanyika nchini Morocco.
Mechi ni saa 1:00 Usiku Alhamisi.