Mshambuliaji wa Tabora United, Heritier Makambo ‘Mzee wa Kuwajaza’ amesema kuna mabadiliko makubwa ya ubora katika Ligi Kuu Bara kulinganisha na misimu kadhaa nyuma alipokuwa na kikosi cha Yanga.
Makambo ameitumikia Yanga kwa misimu miwili tofauti baada ya kuuzwa Horoya ya Guinea na baadaye akarejea tena nchini na kuondoka kwenda Uarabuni kabla ya hivi karaibuni kurudi kujiunga na Nyuki wa Tabora ambako tayari ameshafunga bao moja na kuasisti jingine walipoizamisha Namungo 2-1.
Akizungumza nasi, Makambo alisema kuna tofauti kubwa kati ya misimu yake nyuma akiwa na Yanga na ligi ya sasa, ambapo ameweka kuwa wazi imekuwa bora na ya ushindani bila kujali ni timu gani anakutana nayo.
“Nimerudi nina furaha na maisha ya Tanzania siku zote naamini katika upambanaji licha ya ugumu niliouona kwenye mechi moja niliyocheza na kushuhudia kwa macho baadhi ya michezo, nimebaini utofauti mkubwa uliopo tofauti na misimu iliyopita,” alisema Makambo.
“Kuna utofauti mkubwa kuanzia uwekezaji, timu zote zimesajili wachezaji wa kigeni tofauti na misimu ya nyuma ambayo timu za Yanga, Simba na Azam ndizo zilizokuwa na wachezaji wa kigeni lakini sasa uwekezaji umefanywa kwa timu nyingi zaidi ambazo nazo zimeweka nyota wa kigeni.”
Makambo akizungumzia malengo ya msimu huu, alisema anatamani kufikia rekodi yake ya msimu wa kwanza ndani ya Yanga ambao alipachika mabao 17.
“Natambua ugumu uliopo, lakini malengo yangu ni kupambana kufikia rekodi niliyoiandika msimu wa 2018/19 kwa kuifungia Yanga mabao 17 na kupata nafasi ya kuonekana na kutimkia Horoya.” alisema mchezaji huyo.
“Natambua matarajio makubwa waliyonayo mashabiki wa Tabora United juu ya kikosi chao kwa msimu huu hasa kutokana na usajili uliofanywa nikiwepo mimi ambaye wamepata kunishuhudia nikiwa Yanga.”
Makambo na kikosi hicho cha Tabora mchana wa jana walikuwa uwanjani mjini Tabiora kuikaribisha Kagera Sugar katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara iliyokuwa imesimama kupisha kalenda ya Fifa kwa ajili ya mechi za timu za taifa.