Kocha Kumekucha...Ibenge Atajwa Azam FC

Kumekucha...Ibenge Atajwa Azam FC


Baada ya Azam FC kuonekana imegonga mwamba kwa kocha Nasreddine Nabi, anayeinoa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, inaelezwa kuwa kwa sasa nguvu imehamishiwa kwa Mkongoman, Florent Ibenge wa Al-Hilal Club mwenye CV kubwa Afrika.


Klabu hiyo ilihitaji huduma ya Nabi kutokana na alichokifanya katika timu mbalimbali (2013), Al-Ahly Benghazi, Al-Hilal, Ismaily, Al-Merrikh, Yanga na FAR Rabat, lakini mipango inaelezwa ni kama imekwama kwani ndo kwanza kaanza kazi Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na sasa wameamua kumnyemelea Ibenge.


Uongozi wa timu hiyo, unadaiwa kuanzisha mchakato wa haraka wa kuzungumza na Ibenge, ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akihusishwa na klabu mbalimbali za hapa nchini kama Simba na Yanga.


Chanzo cha ndani cha klabu hiyo, kinasema mazungumzo baina ya Azam na Ibenge yanaendelea na pesa siyo ishu kwao, lengo ni kujenga timu ya kunyakua mataji na kufanya vizuri kimataifa, viongozi wanaamini jukumu hilo kocha huyo analiweza.


“Mazungumzo yanaendelea baina yetu na Ibenge, kwani awali tulianza na Nabi ambaye licha ya kumpa pesa ndefu aliikataa,” kilisema chanzo hicho na kuongeza; “CV ya makocha ambao tumewafuata ni kubwa mfano Nabi aliijenga Yanga ndio maana hadi leo inafanya vizuri, ukija kwa Ibenge anachokifanya katika timu mbalimbali za Afrika ni kikubwa, endapo dili likikamilika tutafurahi na tutaona hatua ya malengo yetu.”


Lengo la kumhitaji Ibenge, Azam inataka kuachana na Youssouf Dabo aliyeisaidia timu hiyo msimu uliopita kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara na kukata tiketi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa raundi ya awali na APR kwa jumla ya mabao 2-1 kisha kutoka suluhu na JKT Tanzania katika ligi.


Kwa sasa Ibenge yupo nchini na timu ya Al Hilal ambayo juzi jioni ilitoka sare ya 1-1 na Simba katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC, huku akibebwa na wasifu wake mkubwa katika soka la Afrika, japo Ofisa Habari wa Azam, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alipoulizwa juu ya dili hili, alijibu kwa kifupi; “Hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa, endapo kama lipo basi itajulikana mbele ya safari.”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.