KAZINI KWA BALEKE KUNA KAZI, NANI AKAE NJE BALEKE ACHEZE?

 

KAZINI KWA BALEKE KUNA KAZI, NANI AKAE NJE BALEKE ACHEZE?

Kazini kwa mshambuliaji wa kimataifa wa DR Congo, Jean Baleke kuna kazi. Unajua kwa nini? Ni kutokana na viwango vya Clement Mzize na Prince Dube ambao wanaonekana kufiti vilivyo katika safu ya ushambuliaji ya Yanga kwa sasa chini ya kocha Miguel Gamondi.


Pia kumbuka yupo Mzambia, Kennedy Musonda ambaye ana msimu wa tatu kikosini, huku akitumika mara kadhaa kitokea benchi.


Kinachoendelea kwa Baleke aliyesajili msimu huu akitoka Libya alipokuwa kikipiga baada ya kutemwa na Simba dirisha dogo la msimu uliopita akiwa ameifunga mabao manane ni anapaswa kujitafuta ili kurejesha heshima aliyokuwa nayo kwa mashabiki wa soka nchini kabla ya kuondoka kwenda nje.


Straika huyo Mkongomani mchezo uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE hakuwa hata katika orodha ya wachezaji wa akiba, kimezua mjadala kwa mashabiki na wachambuzi wa soka nchini, licha ya awali ilionekana kama angeleta chalenji kubwa kwa kina Musonda na Mzize aliowakuta kikosini.


ISHU MFUMO


Mfumo wa uchezaji wa Yanga chini ya Kocha Gamondi unazingatia sio tu uwezo wa kufunga mabao, bali pia umuhimu wa timu kucheza kwa pamoja, hasa katika kupanga mashambulizi na kujilinda.


Mzize na Dube wameendana na mfumo huu kwa kiasi kikubwa kwa kuwa sio tu wanacheza kama washambuliaji wa mwisho, pia wanashuka chini kusaidia timu katika kutengeneza nafasi kwa wachezaji wenzao. Wote wawili wana uwezo wa kushiriki kwenye ujenzi wa mashambulizi na hata kuzuia kwa kuanzia juu.


Hii inawafanya kuwa washambuliaji wa kisasa wanaochangia zaidi ya kufunga mabao.


Kwa upande mwingine, Jean Baleke, licha ya kuwa na rekodi nzuri ya ufungaji akiwa na timu ya Simba, anakabiliwa na changamoto ya kufiti katika mfumo wa sasa wa Yanga.


Baleke ni mshambuliaji ambaye nguvu yake kuu ni kumalizia mashambulizi, lakini kwa mujibu wa Kocha Gamondi, timu inahitaji zaidi kutoka kwa washambuliaji wake wa mwisho.


Uwezo wa Baleke wa kushiriki katika majukumu mengine kama kuzuia mashambulizi au kutengeneza nafasi kwa wenzake unaonekana kuwa mdogo ukilinganisha na Dube na Mzize.


GAMONDI AFUNGUKA 


Kocha Gamondi ameweka wazi mtazamo wake kuhusu nafasi ya Baleke akisema: “Swali kuhusu Baleke ni zuri sana na nashukuru kwa kuuliza. Soka ni mchezo wenye ushindani mkubwa. Nina wachezaji watatu kwenye nafasi hiyo na tunahitaji kufanya maamuzi ya busara kuhusu nani aanze. Baleke ni mchezaji mzuri sana, lakini anahitaji muda zaidi wa kuzoea mfumo wa timu na kuelewa majukumu yake kikamilifu.”


Gamondi aliendelea kusema kuwa Baleke bado ni mchezaji mpya na inachukua muda kujifunza mifumo ya timu.


“Baleke ni mpya, anahitaji muda wa kuzoea, kuelewa mfumo wetu wa mchezo na jinsi tunavyocheza. Ni ngumu kumpa nafasi moja kwa moja kwa sababu tunahitaji uwiano kwenye kikosi, hasa wakati wa kupanga wachezaji wa akiba ambapo lazima tuwe na mabeki, viungo watatu, na washambuliaji wawili.”


Kocha huyo pia alifafanua kuwa uamuzi wa kutomjumuisha Baleke kwenye mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE unatokana na hali halisi ya ushindani kwenye timu.


“Ushindani kwenye nafasi ya Baleke ni mgumu. Tunahitaji kufanya maamuzi magumu na kwa sasa tunafanya kazi kila siku kumtayarisha kuwa tayari kuchukua nafasi yake pindi atakapokuwa amezoea kikamilifu.”


MSIKIE MTAALAMU Mchambuzi wa soka na kocha wa zamani wa Gwambina FC na Mtibwa Sugar, Mohamed Badru, anaamini kuwa changamoto ya Baleke inatokana na mabadiliko katika mahitaji ya makocha wa kisasa.


Badru anasema kuwa makocha wengi sasa wanapendelea wachezaji wenye uwezo wa kufanya mambo mengi uwanjani, tofauti na mshambuliaji wa kati kiasili ambaye mara nyingi majukumu yao huwa ni kufunga tu.


Kwa mujibu wa Badru, Baleke ana sifa nzuri za mshambuliaji wa namba tisa kiasili kabisa, lakini anapaswa kuboresha uwezo wake wa kuchangia zaidi katika uchezaji wa timu. “Baleke ni namba tisa wa asili, na siku hizi wachezaji wa aina yake wanapotea kwa sababu makocha wengi wanahitaji wachezaji wenye uwezo wa kufanya zaidi ya jambo moja. Uwezo wake wa kufunga ni mzuri, lakini changamoto yake ni kubeba majukumu mengine ya timu,” alisema Badru.


JAMBO MUHIMU Japo Baleke amekuwa na changamoto ya kuendana na mfumo wa Gamondi, bado kuna matumaini ya kuona kilicho bora kutoka kwake na kuchangia zaidi kwenye timu. Kama Gamondi alivyosema, Baleke ni mchezaji mzuri, lakini anahitaji muda wa kuzoea na kuelewa majukumu yake mapya ndani ya kikosi cha Yanga.


Katika mpira wa kisasa, wachezaji wanatakiwa kuwa na uwezo wa kucheza zaidi ya nafasi moja na kushiriki katika majukumu ya timu nzima. Kwa hiyo, Baleke atahitaji kuongeza bidii katika mazoezi, kuzingatia maagizo ya kocha na kuonyesha kuwa anaweza kubadilika ili kuendana na mahitaji ya mfumo wa timu.


Kwa sasa, Mzize na Dube wanaonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi kutokana na uwezo wao wa kujituma katika nyanja zote za uchezaji, lakini kama Baleke atachukua hatua sahihi na kufanya kazi kwa bidii, bado ana nafasi ya kuwika na kufanya maikubwa akiwa na kikosi hicho cha Wananchi.


Mzize na Dube ambao wameonekana kutoa mchango mkubwa wa mabao ya Yanga msimu huu inatoa picha ya wazi kwamba ni ngumu kwa Gamondi kufikiria kumtumia mchezaji mwingine wa eneo hilo kama sehemu ya majaribio.


Wawili hao pekee msimu huu katika mechi nane za mashindano yote ambapo timu imefunga mabao 24 wao wamefunga jumla ya mabao tisa, Mzize (5) na Dube (4).


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad