Kochi Nabi 'Tumechukua Tahadhari zote Dhidi ya Marumo Gallants
Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Mohammed Nabi, amesema mchezo wa Mkondo wa Pili wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Marumo Gallants, watacheza kwa tahadhari kufanikisha malengo ya kusonga mbele.
Young Africans ipo mbele kwa mabao 2-0, baada ya kushinda nyumbani jijini Dar es salaam katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Nusu Fainali, wafungaji wakiwa ni Stephane Aziz KI na Bernard Morrison.
Nabi amesema kila mchezo ambao wanacheza ni muhimu kupata ushindi ili kufikia malengo ya kusonga mbele.
“Kukamilisha mchezo wa kwanza kwa ushindi haina maana kwamba kazi imekwisha bado kuna mchezo mwingine wa pili ambao ni muhimu.
“Tahadhari ni muhimu kwani sisi tumeshinda nyumbani na tunawafuata kwao, tunaamini watakuwa wanahitaji kushinda kama ambavyo tunahitaji kushinda, hivyo ushindani utakuwa mkubwa,” amesema
Keshokutwa Jumatano (Mei 17), Young Africans inatarajiwa kumenyana na Marumo Gallants katika Uwanja wa Royal Bafokeng mjini Rustenburg, mshindi wa jumla wa mchezo huo atasonga hatua ya Fainali ya la Shirikisho Barani Afrika.