Aliyekuwa nahodha wa klabu ya Simba Sc Mohamed Hussein (Zimbwe Jr) ameaga rasmi klabu hiyo baada ya mkataba wake kumalizika na kutokuongezwa ambapo Kupitia ujumbe aliouandika katika ukurasa wake Mohamed ameushukuru uongozi, benchi la ufundi, Wafanyakazi wa klabu na Mashabiki wa Simba Sc kwa sapoti waliompa kwa kipindi chote alichoitumikia timu hiyo kwa takribani miaka 11.
Katika ujumbe wake Mohamed Hussein alieleza kuwa maamuzi ya kuondoka Simba SC yamelenga maendeleo na maslahi yake binafsi pamoja na kukuza weledi wake wa soka ambapo amesisitiza kuwa kuipigania nembo ya Simba Sc kulikuwa ni heshima kubwa kwake.
Huku akiaga rasmi tetesi zimeanza kuzagaa kwamba beki huyo mahiri yupo mbioni kujiunga na Yanga SC, wapinzani wakubwa wa jadi wa Simba ingawa bado hakuna taarifa rasmi kutoka klabu husika, Mashabiki na Wachambuzi wa soka wanaendelea kufuatilia kwa karibu mustakabali wa nyota huyo.