Wakati kukiwa na mijadala kuhusu wachezaji wa ligi mbalimbali za soka nchini kuhusika katika michezo ya kubashiri (betting) na kupanga matokeo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amefichua kuwa ameshawanasa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wakijaribu kuihujumu.
.
Kauli hiyo ya kushtua ya Mtanda ambaye pia ni mlezi na mshauri wa timu hiyo, aliitoa juzi jijini Mwanza wakati wa hafla ya chakula cha usiku na wachezaji, benchi la ufundi na menejimenti ya klabu hiyo kuelekea michezo ya mzunguko wa pili Ligi Kuu.
.
Alisema tabia hiyo kwa sasa ni ugonjwa mkubwa katika soka la Tanzania ambapo ili kukomesha tabia hiyo tayari wamewasilisha majina ya wachezaji wote wa kikosi chao kwenye Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kufuatilia nyendo zao.
.
“Hivi vitu vipo na vina tokea sasa wewe tunakulipa mshahara Sh3 milioni mpaka Sh4 milioni halafu unabashiri Pamba ipoteze. sasa nimepeleka namba zenu TCRA yeyote atakayebeti nitaona na ni rahisi kwangu,” alisema Mtanda.
.
“Kuna mchezaji mwenzenu nilimwambia mlipokwenda kucheza na Namun go alikuwa anashawishi wenzake muuze mechi na ukitaka ushahidi nitakupa nikamkanya aache. Nawaonya muache kwa sababu ushahidi ninao na sitaki mambo haya yaendelee.
.
“Sitaki kutaja majina lakini nimeshaongea na baadhi yenu wengine wanatumia simu za wake zao kupokelea hiyo miamala, hivyo nawaonya hii ni timu ya taasisi ya serikali ambayo fedha nyingi zinatumika ambazo zingeenda kwenye miradi mingine.
.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, alisema menejimenti imekubaliana kutafuta fedha za motisha na kuziweka kwenye akaunti ili ziwe tayari muda wote na wachezaji wapewe kianzio (advance) kabla ya mchezo.