HAKIKA Yanga ilistahili kutolewa. Katika jioni kama ya juzi haikuwa na sababu yoyote ya msingi ya kwenda robo fainali ya michuano ya CAF na wana mambo mengi ya kujifunza kabla ya kutawala soka la Afrika kwa mfululizo kama timu kubwa zinavyofanya.
Ilikuwa jioni nyingine mbovu kwao. Mechi tatu za nyumbani imepata alama nne badala ya tisa. Aibu iliyoje. Soka la Afrika huwa linatawaliwa na timu za nyumbani. Yanga haikufanya hivyo katika mechi ambayo ilihitaji pointi tatu kwa machozi, jasho na damu.
Ndani ya uwanja ilishangaza kuona Kocha Saed Ramovic akianza pambano bila ya Pacome Zouzoua na Clatous Chama dakika 45 za mwanzo. Yanga ilikosa ubunifu katika eneo la ushambuliaji. Ilianza na Prince Dube, Clement Mzize, Stephane Aziz Ki na Kennedy Musonda. Ilikosa ubunifu katika lango la wapinzani wao MC Alger ambao kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho ilikuwa inatafuta sare.
.Hawakuonana, hawakutafutana, kila mtu alikuwa anataka kuwa shujaa wa pambano hilo kwa sababu Yanga walikuwa wanahitaji pointi tatu muhimu kufuzu. Lilikuwa jambo la kisaikolojia zaidi kwa wachezaji kutulia na kutafuta nafasi kwa timu sio kwa ufalme wa mchezaji mmoja mmoja.
.Unaweza kuwalaumu Mzize na Dube, lakini kuna nafasi ngapi za wazi walipoteza? Hakuna. Sina hofu ya kusema hata kama mwamuzi angeongeza dakika 40 zaidi katika muda wa nyongeza bado Yanga wasingefunga.”
— Legend Edo Kumwembe. [via Mwananchi]