Wachezaji Wazawa wa Tanzania |
Kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Hispania, Rodrigo Hernández Cascante maarufu zaidi kama Rodri, amegonga vichwa vya habari baada ya kauli yake ya kishujaa kwa mamlaka za mpira duniani.
Akiwasilisha hisia za wachezaji wengi kama siyo wote wa Ulaya, Rodri amelalamikia utitiri wa mechi unaotokana na kupanuliwa kwa mashindano.
“Nadhani wachezaji tunakaribia kufanya mgomo. Naamini hata ukimuuliza mchezaji yeyote atasema hivyo hivyo.”
Haya siyo maoni ya Rodri au mwingine yeyote. Naamini ni maoni ya jumla ya wachezaji wote.
Shirikisho la Soka Ulaya, UEFA, limebadilisha muundo wa mashindano yake makubwa kwa ngazi ya vilabu, Ligi ya Mabingwa.
Katika muundo mpya, idadi ya timu imeongezeka kutoka 32 hadi 36.
Kuongezeka kwa timu maana yake mechi pia zimeongezeka.
Shirikisho la Soka la Kimataifa, (FÄ°FA), nalo limefanya mabadiliko ya muundo kwenye mashindano yake makubwa zaidi kwa ngazi za Klabu, Klabu Bingwa ya Dunia.
Katika muundo mpya, idadi ya timu imeongezeka kutoka 7 hadi 32.
Kuongezeka kwa timu maana yake pia na mechi zimeongezeka.
Kwa jumla hii ina maana kwamba msimu wa 2024/25, timu kama Manchester City anayoitumikia Rodri, inaweza kucheza mechi hadi 85, kutegemea na namna timu itasonga mbele kwenye mashindano.
Katika hali ya kawaida, mchezaji anapaswa kucheza mechi 45 hadi 50 kwa mwaka, lakini sasa anaweza kucheza hadi mechi 85, hiki ndicho kinachoweza kuwafanya wachezaji wagome.
Japo kugoma kunaweza kusitokee, lakini kimsingi wachezaji wanapaza sauti zao juu ya mzigo wanaoenda kuubeba kuanzia msimu huu.
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, akaibuka kuwatetea wachezaji kwa kusema hii siyo sawa.
Mpira unapaswa kuangaliwa upya kwa sababu lengo ni kucheza mechi chache ili kupunguza majeraha.
Lakini vilabu na waandaaji wa mashindano wanadai kwamba wanabeba mzigo mkubwa wa gharama za mashindano hivyo watahitaji pesa kutoka kwenye mashindano ili kuwalikipa wachezaji.
Hivyo wameamua kubadilisha muundo kwa lengo la kuzalisha pesa zaidi kwa sababu mechi zikiwa nyingi zitaleta wadhamini zaidi na kuleta pesa zaidi.
Carlo Ancelotti analipinga wazo hili akisema endapo wachezaji wenyewe wangeshirikishwa, yawezekana yangekuja majibu tofauti.
Lengo ni wachezaji kucheza mechi chache zaidi. Kama kupunguza mechi kutamaanisha kupunguza mishahara siamini kama wachezaji watakuwa na tatizo kushusha mishahara yao ili wacheze mechi chache zaidi.
NANI AWATETEE WACHEZAJI WETU
Wakati wachezaji wa Ulaya, ambako kuna miundombinu bora zaidi ya kuchezea na hata tiba, wanalalamikia idadi ya mechi, huku kwetu hakuna anayepaza sauti.
Kwetu miundombinu ya kuchezea ni duni sana. Mipango ya lishe ni duni. Vifaa vya mazoezi na programu za kurudisha mwili kwenye hali yake ya kawaida baada ya mazoezi magumu au mechi ngumu nayo ni duni.
Na hata tiba pia ni duni, lakini tuna mechi zinazozaliwa kila uchao na zinachezwa kwenye ratiba iliyopangwa vibaya.
Hebu angalia ratiba hii ya Azam FC
Septemba 19
KMC vs Azam FC
Septemba 22
Azam FC vs Coastal Union
Septemba 26
Azam FC vs Simba
Septemba 29
Mashujaa vs Azam FC
Oktoba 3
Namungo vs Azam FC
Kutoka mechi ya KMC hadi mechi ya Coastal Union kuna saa pungufu ya 72, kinyume na maelekezo ya FIFA.
Kutoka mechi ya Simba hadi mechi ya Mashujaa kuna saa pungufu ya 72, na bado kuna safari ya takribani kilomita 1000.
Halafu baada ya siku tatu, kuna mechi ya Namungo, umbali wa kilomita takribani 1000 tena.
Haya ndiyo maisha ya wachezaji wa Tanzania. Ratiba imeshonana, hakuna muda wa kupumzika na katikati yake kuna safari ndefu.
Kwa miundombinu yetu ya usafiri, ukirejea na matatizo ya tiba, lishe na kurudisha mwili katika hali ya kawaida, utaona wachezaji wetu wapo kwenye hatari kubwa sana.
Juu ya hayo, kuna mashindano yanazaliwa katikati yake na kuongeza idadi ya mechi.
Kombe la Mapinduzi, Kombe la Muungano, mechi za timu ya taifa na kadhalika.
Haya yote yanafanyıka pası na mtu hata mmoja kusimama na kupaza sauti kwa niaba yao.
Hii ni kwa sababu yawezekana wao wenyewe hawajui hatari iliyopo mbele yao.
Wanacheza kwenye viwanja vibaya ambavyo ni hatari kwa kazi yao, kisha hawapati muda wa kutosha wa kupumzika, na hawapati programu nzuri za kurudisha mwili katika hali ya kawaida…na wakiumia hawapati tiba nzuri.
Matokeo yake wachezaji wanaonekana wameisha wakiwa na umri mdogo tu…
Nani awapiganie wachezaji wetu?