Kuna vitu vingine inabakia kuwa ni siri ya Mwenyezi Mungu. Nimeifuatilia Yanga kwa miaka mingi sasa, inatabia ya kuanza mashindano au ligi katika Low Gear au Low Key.
Inaweza kuanza kwa kufungwa, kutoka sare au ushindi wa tia maji tia maji, halafu taratibu inaanza kushika kasi. Miaka ya 1980's kuna wakati kulikuwa na imani kuwa Yanga ikianza vibaya msimu basi lazima ichukue ubingwa.
Klabu ya Al Ahly pia inatabia ya kuanzia gia ya chini na kuanza kushika kasi taratibu, kuna msimu unaweza kudhani watatoka patupu lakini haiwi hivyo. Tabia hii hata Manchester City wamekuwanayo kwa miaka ya karibuni.
Yanga imeuanza msimu na mapungufu haya: 1. KUPUNGUA KWA KASI Timu inafanya transition taratibu sana isipokuwa kwa matukio machache ya mchezaji mmoja mmoja mfano Boka na Paccome, hawa wanajitahidi sana kuipa mwendo timu.
2. KUCHELEWA KUPORA MIPIRA Kuna baadhi ya michezo timu imekuwa inachelewa kupora mipira toka kwa wapinzani, hili lilionekana zaidi mechi mbili za Wahabeshi au nyingine ambazo Mudathir Yahya hakuwemo uwanjani.
3. KUKOSA MAGOLI YA WAZI Wachezaji wa Yanga kila mmoja analazimika kukimbia kilometa nyingi, hili huchangia ukosaji magoli. Wafungaji wazuri mara nyingi ni wale wasiobebeshwa majukumu mengi hivyo wanakuwa na utulivu wa kiakili.
4. PASI KUPOTEA KIRAHISI Kuna baadhi ya wachezaji miili yao haijafunguka tangia warudi msimu huu hivyo wanashindwa kuendana na rhythm ya timu.
5. KUWATUMIA WACHEZAJI KATIKA MAENEO YASIYO SAHIHI Kuna baadhi ya mechi baadhi ya wachezaji wametumiwa katika maeneo ambayo hawaipi timu ufanisi unaotakiwa Nzengeli kutokea kulia, Mzize kushambulia kutokea kati au Chama kucheza kiungo cha chini.
6. KUWARUHUSU WAPINZANI KUSHAMBULIA KIRAHISI Kuna namna msimu huu lango la Yanga linafikiwa kirahisi ingawa wapinzani hawatumii nafasi. Kwa kuwa ni mwanzo wa msimu, ngoja tuone nini kitatokea.
CLEMENT MZIZE Kuelekea kuanza kwa msimu huu kulikuwa na tetesi nyingi za Mzize kutakiwa huku na kule. Nikadhani atapagawa na kupoteza mwelekeo badala yake anazidi kuwa bora. Labda anaamini nyama ziko chini.