Achana na Habari ya DABI, Yanga Mawazo Yao Yoote Yako Huku....
Klabu ya Yanga imesema kutokana na ubora wa kikosi ilichonacho pamoja na uzoefu, itavuka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kwenda robo fainali kwenye Kundi A lililopangwa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Andre Mtine, amesema si kwamba anazidharau timu zingine, lakini anaziona zimo ndani ya uwezo wao, ingawa kwenye soka lolote linaweza kutokea.
Mtine ameongea hayo baada ya Yanga kupangwa Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa na timu za TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, MC Alger ya Algeria na Al Hilal ya Sudan.
Amefafanua kuwa pamoja na ubora ambao timu hizo zinao, lakini si kama Mamelodi Sundowns, Al Ahly, Esperance, Raja Casablanca, Wydad Casablaca, Zamalek na nyingine kubwa na tishio barani Afrika.
“Kwa nilivyoona kundi ni kwamba tunavuka makundi, tuna timu nzuri, ngumu na yenye wachezaji bora wenye viwango na kwa sasa tuna uzoefu pia, pamoja na kwamba si kazi rahisi na si kwamba nazidharau timu zingine, lakini bado zipo ndani ya uwezo wetu, hizi si zile timu tishio barani Afrika ambazo ukipangiwa nazo unaona ni lazima ufanye kazi ya ziada,” alisema.
Kwa upande wa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Alex Ngai, yeye amesema haoni kama ni kundi jepesi, lakini matarajio yake ni kuona Yanga ikivuka hatua hiyo. “Hakuna timu nyepesi kwenye hili kundi, ila sisi mipango yetu ipo vile vile, malengo na matarajio ni kuvuka kwanza hili kundi, baadaye tutaona tunakwendaje huko mbele,” alisema.
Wakati huo huo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema maandalizi kuelekea kwenye mchezo wa dabi dhidi ya Simba, Oktoba 19, mwaka huu, yameanza rasmi.
Alisema Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, ameanza mazoezi na wachezaji waliosalia ambayo hawajaitwa kwenye vikosi vya timu za taifa.
“Timu imeanza kujiandaa na mazoezi kuelekea Oktoba 19 ambapo tutacheza dhidi ya Simba, baadhi ya wachezaji wetu wapo kwenye vikosi vya timu ya taifa, lakini waliobaki wanaendelea na maandalizi.
Ila tunawaombea wachezaji wetu waliokwenda kwenye timu za taifa warejee wakiwa salama bila majeruhi kwani tuna mechi ngumu ya dabi, tunataka kuvuna pointi sita kwenye michezo yetu miwili ya mwezi Oktoba, kwani baada ya hiyo tutacheza dhidi ya JKT Tanzania,” alisema Kamwe.