Hali sio shwari ndani ya kikosi cha Coastal Union kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo ya Ligi Kuu Bara inayoendelea kuyapata huku kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Lazaro akieleza ni upepo mbaya wanaokutana nao na sio vinginevyo.
Kichapo cha juzi cha bao 1-0, dhidi ya Azam FC kimeifanya timu hiyo kupoteza michezo mitatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara kati ya minne iliyocheza huku ikiambulia sare mmoja tu, jambo linaloonyesha wazi hali ya kikosi hicho sio ya kuridhisha.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Lazaro alisema wachezaji wanajitahidi kuonyesha uwezo wao uwanjani japo kinachotokea hata yeye kinamshangaza, huku akiwataka mashabiki wa kikosi hicho kuendelea kuwapatia sapoti.
“Inaumiza lakini muda mwingine ni lazima ukubaliane na hali halisi, wachezaji wanajituma sana katika nafasi zao ingawa tunashindwa kupata matokeo chanya, bado tuna nafasi ya kurekebisha hali iliyopo ambayo ni suala la saikolojia tu kwao,” alisema.
Lazaro aliongeza kuwa timu hiyo itakapopata ushindi anaamini itarudi katika mstari mzuri kwa maana ya kutengeneza hali ya morali kwa wachezaji huku akiwapongeza kwa kujitoa sana kwa asilimia 100 kwenye mchezo na Azam FC, licha ya kupoteza.
Coastal Union ilianza Ligi Kuu Bara msimu huu kwa sare ya bao 1-1, dhidi ya KMC kisha kuchapwa michezo mitatu mfululizo ikianza na 1-0, mbele ya Mashujaa, (2-0) Namungo FC kisha kuchapwa bao 1-0 na Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Kocha huyo amekabidhiwa kikosi hicho kwa muda baada ya Mkenya, David Ouma kutimuliwa Agosti 24 mwaka huu kutokana na kile kilichoelezwa na viongozi wa timu hiyo kutoridhishwa na mwenendo wa matokeo ambayo ilikuwa ikiyapata kipindi chake.
Ouma aliyejiunga na Coastal Union Novemba 9, mwaka jana akichukua nafasi ya Mwinyi Zahera, alitimuliwa baada ya timu hiyo kupoteza kwa mabao 3-0, dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola katika mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika.