HADI SASA FEI TOTO AMEIPIGA YANGA MABAO MATATU

 

HADI SASA FEI TOTO AMEIPIGA YANGA MABAO MATATU

Wiki iliyopita habari iliyotawala ulimwengu wa michezo Tanzania ni kauli ya nyota wa Azam FC na Taifa Stars, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuhusu uhusiano wake na rais wa klabu ya Yanga, Hersi Said.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye siku ya vyombo vya habari ya Azam FC, Septemba, Fei Toto alisema ana mawasiliano mazuri na Hersi tofauti na watu wengi wanavyodhani.

Kauli hiyo inakinzana na kauli nyingine kutoka kwa Fei Toto wakati wa harakati zake za kuondoka Yanga zilizoanza Desemba 2022 na kukamilika Julai 2023.

Katika moja ya mahojiano na vyombo vya habari, Fei Toto alisema kisa cha yeye kuondoka Yanga ni maelewano yake mabaya na Hersi Said, kama rais huyo ataondoka Yanga, basi Feitoto angekuwa tayari kubaki klabuni hapo.

Kwa hiyo aliposema ana mawasiliano mazuri na Hersi, akaibua maswali mengi. Pia Fei alikwenda mbali na kusema kama mchezaji anaweza kucheza klabu yoyote ndani au nje ya nchi.

Wachokonozi wa mambo wakarejea mkataba wa mauzo yake kutoka Yanga kwenda Azam FC ambapo kuna kipengele kinachosema;

Endapo Azam FC itataka kumuuza kwenda klabu ya ndani ya Tanzania, basi Yanga waulizwe kwanza kama wako tayari kumnunua – ni hadi watakaposhindwa wao ndiyo klabu nyingine ije.

Kutokana na kipengele hicho, ikaonekana kabisa kwamba ni rahisi Feitoto kurudi Yanga kuliko kwenda Simba, endapo ataondoka Azam FC na kuhamia klabu nyingine hapa Tanzania.

Mambo hayo mawili yakalipua nyoyo za wana Yanga na kuanza kujiaminisha kwamba sasa Fei Toto ‘ameimisi’ Yanga na anajuta.

Ofisa habari wa Yanga haraka haraka akaandika kwenye Instagram yake kuwaomba mashabiki wa Yanga walioacha kumfuatilia Fei Toto kwenye mitandao ya kijamii, waanze kumfuatilia tena.

Roho za wana Yanga zikafunguka na kuanza kumtazama upya Feitoto kwa jicho la kirafiki badala ya chuki kama zamani.

Na hilo ndiyo BAO LA KISIGINO ambalo Feisal Salum amewafunga Yanga. Na kwa bao hilo, Fei Toto sasa anaongoza 3-0 mbele ya Yanga, huku mechi ikiendelea.

Kwanini? Mechi baina ya Feisal Salum na Yanga ilianza Desemba 22, 2022 pale alipopeleka barua ya kuomba kuondoka klabuni kwake, Yanga.

Mechi Hii ilikuwa ngumu sana lakini baada ya dakika tisini Fei Toto akashinda na kuondoka. Hilo lilikuwa bao la kwanza kwa Feisal Salum dhidi ya Yanga.

Klabu hiyo kongwe nchini huamini kwamba kila mchezaji anatamani kuitumikia, kwa hiyo Fei Toto aliposema anataka kuondoka, iliwauma sana.

Wakajaribu kila njia kumbakisha, ikashindikana akaondoka na kuwaacha na hasira.

Hasira hizi zikazaa chuki na dua mbaya dhidi ya mchezaji hiyo kutoka visiwani Zanzibar. Watu wa Yanga wakatamani kumuona anafeli akiwa Azam FC ili waseme, “kiko wapi”.

Lakini kwa bahati mbaya kwao na nzuri kwake, Fei Toto ameng’ara zaidi akiwa na Azam FC kuliko alipokuwa na Yanga.

Msimu wake wa kwanza alifunga mabao 19 kwenye ligi kuu, ilhali alipokuwa Yanga hakuwahi kufikisha angalau nusu ya hayo.

Na siyo tu kufunga mabao kwenye ligi, hata kuwafunga Yanga wenyewe na kuubonda mwingi sana wanapokutana.

Hilo likawa bao la pili kwa Yanga kutoka kwa Feisal Salum.

Mabao haya mawili yakamjengea chuki Feisal Salum mbele ya Yanga ambayo ni familia kubwa sana.

Kila mwanayanga alimuangalia Fei Toto kwa jicho baya, alimuita jina baya na alimsema vibaya.

Kama binadamu, kuna wakati hali hii inakuumiza kisaikolojia. Sasa ili kulegeza nyoyo za wanayanga, ndipo akatoa kauli ile na kweli, mkakati umelipa.

Yanga wenyewe wanahamasishana kukunjua roho zao na kuanza kumuombea dua njema. Hilo ndilo bao la tatu ambalo Fei Toto amewafunga Yanga.

Kama unaweza kumuua mtu kwa asali, kwanini umpe sumu? Fei Toto amewapa Yanga asali, wanailamba huku wanakufa taratibu halafu yeye anarudi kati kushangilia bao la tatu.

Wakati Yanga wanapata matumaini ya kumrudisha Fei Toto Jangwani, watakuja kushtukia kaongeza mkataba na kuendelea kuwadhuru wakikutana.

Full time: Fei Toto 3-0 Yanga

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad