GAMONDI AMKATAA BALEKE 'HAJAKIDHI KWENYE MFUMO WANGU'
Kocha wa Klabu ya Yanga SC Miguel Gamondi amesema inampa ugumu kumchezesha mshambuliaji Jean Baleke kwa sababu itampasa amtoe Clement Mzize au Prince Dube.
Gamondi amesema anajua uwezo wa Baleke lakini kwa sasa Prince Dube na Clement Mzize wanakidhi mahitaji yake katika mfumo wake kuliko Baleke ambaye bado ni mgeni na anahitaji kuujua mfumo, na sio kitu rahisi.
Aidha, Gamondi amesema kuwa anajisikia vibaya kutomchezesha Mkongomani huyo aliyesajiliwa na Yanga msimu huu akitokea nchini Libya.
“Kwenye mfumo wangu ninataka mshambuliaji mmoja, Dube anafunga mabao na anafanya vizuri, Mzize anafunga mabao na anafanya vizuri, nikimuweka Baleke maana yake nimtoe Dube au Mzize, kwa nini? Hakuna sababu ya ziada.
“Ninachoweza kuseme kuhusu Baleke ni kwamba nina utajiri wa wachezaji wengi wazuri kwenye nafasi yake. Kama binadamu najisikia vibaya kwa sababu ninataka kumpa nafasi baleke lakini nikimuweka Baleke ninatakiwa nimtoe mzize au Dube.
“Mimi sio mjinga kumuacha mchezaji nje, lakini ninatoa kipaumbele kwa wachezaji hapa mwanzoni mwa msimu. Hakuna mtu anawajua wachezaji wangu zaidi yangu mimi kocha wao, ninafanya nao mazoezi kila siku, ninawafundiaha kila siku.
“Naweza kusema labda Prince Dube na Mzize wananipa zaidi kwenye mahitaji ya mfumo wangu kuliko Baleke, na Baleke ni mgeni ni mgeni anatakiwa kufahamu mfumo na kuzoea mazingira ya timu na muunganiko wa timu, sio kazi nyepesi.
“Ninajisikia vibaya kuhusu Baleke kwa sababu hata mchezo uliopita (dhidi ya CBE) sikuweza kumpanga hata sub kwa sababu ninatakiwa kupanga mabeki watatu, viungo watatu na washambuliaji watatu au wawili. Kwenye timu kama Yanga unawechazji wengi wenye ubora, mchezaji akija Yanga anatakiwa apambane.
“Mchezo uliopita Aziz KI alikuwa benchi na Dube alikuwa benchi na walikubali kwa sababu kuna competition kwenye nafasi zao. Kwa sasa jezi ya Yanga ina thamani kubwa kupata nafasi,” amesema Gamondi.