Mdomo wa Ahmed Ally Atamponza Mchezaji Steven Mukwala
Usajili wa mshambuliaji aliyefanya vizuri sana kule Ghana katika Ligi Kuu ya nchi hiyo, Steven Mukwala ulishereheshwa vilivyo na Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.
Mshambuliaji huyo hakuwa mwingine bali ni raia wa Uganda, Mukwala na msimu uliopita alifunga mabao 14 katika mechi 28 za Asante Kotoko katika Ligi Kuu ya Ghana, huku akipiga pasi mbili za mwisho.
Takwimu
Takwimu hizo zikamuibua rafiki yangu, Ahmed Ally aliyeutambulisha usajili wa Mukwala kwa mbwembwe sana kwamba ni mfungaji hasa na tishio zaidi katika kuziona nyavu za timu pinzani, hivyo watakaokabiliana naye kazi watakuwa nayo.
Kwa Ahmed alikuwa anatimiza wajibu wake wa kuwafanya mashabiki wa Simba wasiuanze msimu kinyonge na wasiutilie shaka usajili ambao uongozi umeufanya kwa msimu uliozinduliwa jana kwa mechi za Ngao ya Jamii kabla ya Ligi Kuu 2024-2025 kuanza wiki ijayo.
Msemaji huyo alituaminisha Mukwala atafunga sana hasa mabao yatokanayo na mipira ya juu na atafumania nyavu bila hata kuruka kwa mipira ya vichwa kwa vile umbile lake kubwa.
Lakini kwa upande mwingine sifa za Ahmed ambazo Mukwala alizipata baada ya kutambulishwa zikawafanya wengi waweke matarajio makubwa naye wakiamini atakuwa mkombozi wa Simba pale mbele baada ya kupita misimu mitatu mfululizo bila ya kuwa na mshambuliaji asilia ambaye amefanya vizuri.
Matarajio ya Mashabiki
Matarajio hayo ndiyo yanatengeneza presha ambayo Mukwala kama asipokuwa makini katika kukabiliana nayo inaweza kumfanya ama achelewe au asitimize matarajio makubwa ambayo mamilioni ya mashabiki wa Simba wameyaweka kwake katika msimu wa 2024/2025.
Namwona Mukwala akiwa na kibarua kigumu zaidi katika kikosi cha Simba pengine kuliko hata wengine aliosajiliwa nao dirisha hili la usajili kwa vile sifa alizopata na namba anayocheza vinamkaanga mbele ya mashabiki.
Ni rahisi kumtetea kiungo au beki lakini sio mshambuliaji kwa vile yeye kazi yake inapimwa kwa mabao. Masuala ya mikimbio mizuri sijui na kukaa kwenye nafasi sio ya msingi sana kwa wanasimba kuliko mabao ambayo tayari wameshaaminishwa Mukwala atawapatia.