Hapa Ndiyo Lilipo Anguko la SIMBA, Kujisifia Kwa Kiwango Badala ya Magoli.....

 

Hapa Ndiyo Lilipo Anguko la SIMBA, Kujisifia Kwa Kiwango Badala ya Magoli.....

 Hapa Ndiyo Lilipo Anguko la SIMBA, Kujisifia Kwa Kiwango Badala ya Magoli.....

Mchezo wa saba wa ngao ya jamii baina ya watani wa jadi wa Tanzania, Yanga na Simba, umeamuliwa na bao la dakika ya 43 la Mbappe wa Kindu, Maxi Nzengeli.


Kama ilivyo kwa watani wa jadi, matukio ya imani za kishirikina hutawala kabla na wakati mwingine wakati wa mchezo, na kwenye mchezo huu yalikuwepo pia.


Tofauti kidogo kwa kulinganisha na mechi kadhaa huko nyuma, safari ‘boli’ lilitembea…hasa dakika 30 za kwanza.


Kulikuwa na vitu vingi vya kuvutia, vikiwemo ubunifu, ufundi na mbinu pia.


Lakini kituko kikubwa ni baada ya mchezo licha ya kufungwa 1-0, Simba walionekana kuwa na furaha zaidi ya washindi, Yanga SC.


Akiongea na waandishi wa habari baada ya mechi, Mkuu wa Idara ya Habari Simba, Ahmed Ally, alikiri dhahiri kwamba licha ya kufungwa, wao wana furaha kubwa sana.


Eti Simba wanasema timu yao ilicheza vizuri hivyo wameridhika na kiwango. Eti walitarajia dhahama, kwamba wangefungwa mabao mengi, lakini wamepambana hadi kufungwa 1-0.


Hizi mimi naziita dalili za kuanza kuanguka kwa bwana mkubwa ndiyo, bwana mkubwa, Simba SC.


Ikiwa ni moja ya vilabu vikongwe zaidi katika vilivyo sasa hapa nchini, Simba ni moja ya vilabu viliyofanikiwa zaidi hapa nchini.


Ni moja ya klabu viliyoshinda mataji mengi zaidi hapa nchini. Ni moja ya klabu viliyozifunga zaidi timu pinzani hapa nchini.


Mbaya zaidi, mechi iliyo kwenye mjadala ni dhidi ya watani wa jadi. Mtu unabaki kujiuliza, ule ufahari wa kumfunga mpinzani wako, umepotelea wapi, hadi kuanza kupata furaha kwa vipasipasi?


UTANI WA JADI


Ulimwengu wa soka umejaa mechi za kukata na shoka kila msimu, lakini hakuna mechi zinazosubiriwa kwa hamu kama za upinzani wa jadi.


Hizi ni zaidi ya mechi za kwenye ratiba, haya ni matukio ya kulinda heshima na fahari ya jezi na nembo ya klabu pamoja na mashabiki.


Hizi ni mechi zinazogawa familia, ni mechi za vita baina yetu na wao.


Hizi ndizo mechi zinazoufanya mchezo huu uwe ulivyo sasa.


Kila linapokuja pambano la watani wa jadi, watu huwekeana vitu mbali mbali.


Mrisho Ngassa wa Yanga aliwahi kuahidi kuchoma moto nyumba zake endapo asingeifunga Simba kwenye pambano lao la Oktoba 20, 2013. Akafunga.


Safari hii, Mwijaku, mmoja wa wahamasishaji wa mitandaoni na mtangazaji wa redio, aliahidi kumtoa mkewe kwa Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, endapo Simba wangefungwa.


Kuna mtu aliripotiwa kujiua baada ya pambano la kihistoria la 1974 ili kutimiza ahadi aliyoweka kabla ya mchezo. Hizi ndizo mechi za utani wa jadi.


Hizi ni vita za kupigania haki ya kujidai mtaani!


HAIWEZEKANI


Baada ya mechi za aina hii, huwezi kutarajia eti watu kujivunia kiwango, ilhali kuna watu wamepoteza wake zao.


Mechi wa watani wa jadi ni ya matokeo tu, ili kulinda heshima,hakuna kiwango hapo.


Msimu wa 2011/12, Yanga waliifunga Simba 1-0 kwa bao la Davies Mwape kutokana na makosa ya Kelvin Yondani.


Kwenye mechi hiyo, Simba walikuwa bora kila idara, lakini wakapoteza.


Hakuna hata shabiki mmoja wa Simba aliyejivunia kiwango zaidi ya kuumizwa na matokeo.


Lawama zikaenda kwa Emmanuel Okwi kwa kukosa bao la wazi, akiwa na kipa.


Ni fedheha kubwa sana kwa mtani wa jadi kupoteza mchezo halafu kujipongeza kwa kiwango, kiwango chenyewe kile!?


Nadhani Simba inapaswa kuacha kujidanganya na kujitathmini kwa ajili ya mechi zijazo. Hakuna haja ya kujitekenya wenyewe na kucheka kwa kivuli na kiwango ambacho hakikuwepo.


Ukiona klabu kubwa inaanza kujivunia mambo yasiyo na maana, ujue inaanza kuanguka. Simba wanaweza wakawa wanaanza kuelekea huko.


Na kama ni hivyo, hilo litakuwa pigo kubwa sana kwa soka la Tanzania kwa sababu huwezi kuuzungumzia mpira wa Tanzania pasi na kuzigusa Simba na Yanga.


Sasa kama bwana mkubwa Simba anaanza kujitoa kwenye jeuri ya kupigania matokeo na kuanza kujisifia kwa viwango vya uongo, basi ujue anaelekea kubaya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.