Dau la FISTON Mayele Limepanda, Tanzania Hakuna Timu Inatakayo Weza Kumsajili

 

Dau la FISTON Mayele Limepanda, Tanzania Hakuna Timu Inatakayo Weza Kumsajili

Mafarao wa Misri walikamilisha Ligi Kuu yao wikiendi hii iliyoisha. Watu wa ajabu kidogo. Wakati duniani katika maeneo mbalimbali ligi zinaanza wao ndio wametamatisha ligi yao. Sijui wanatumia mfumo upi ambao unawasiganisha na dunia.


Na katika msimu huu ulioisha walikuwa na ugeni wa mchezaji anayeitwa Fiston Mayele. Aliondoka katika ardhi ya Tanzania akiwa shujaa anayetetema. Jina lake liliimbwa kila kona. Hata hivyo, msimu huu ulioisha alipaswa kukifanya alichofanya Tanzania katika ardhi ya Mafarao, Misri.


Hatimaye amefanikiwa kukifanya. Labda tofauti ni kwamba alikuwa anachezea timu ambayo haina mbwembwe nyingi, lakini yenye jina kubwa kwa sasa pale Misri. Pyramids. Mguuni, Mayele ameondoka na mabao 17 ya ligi. Amepiga pasi tano za mabao.


Amekuwa mfungaji bora wa pili nyuma ya staa wa Al Ahly, Wessam Abou Ali. Katika michuano ya FA ya huko amefunga mabao mawili. Bahati mbaya hakufunga katika michuano ya kimataifa. Kifupi Mayele ameondoka na mabao 19 katika msimu wake wa kwanza.


Pyramids hawakukosea kumchukua. Walimchukua mtu sahihi ingawa alianza kwa kusuasua. Hii maana yake nini? Maana yake tunaweza kumsahau Mayele kwa sasa. Najua hapo katikati kulikuwa na uvumi mwingi kuhusu Mayele kurudi nchini.


Kuna walioona uwezekano akarudi zake nchini na kuvaa jezi nyekundu na nyeupe za Simba. Hii ni kutokana kutokuwa katika uhusiano mzuri na klabu yake ya zamani ya Yanga. Waliwahi kushambuliana mitandaoni kwa sababu ambazo mpaka leo hatujui msingi wake.


Niliwahi pia kuambiwa kwamba Azam FC walikuwa wanamnyemelea Mayele. Lakini kifupi zaidi, nani hamtaki Mayele? Hata hao Yanga wenyewe wangekuwa tayari kumalizana na Mayele na kumrudisha nchini kama fursa hiyo ingetokea. Mbona waliwahi kumalizana na Bernard Morrison ambaye aliharibu hapahapa nchini?


Hata hivyo, kwa sasa tunaweza kumsahau Mayele. Dau lake limekwenda juu. Kwa vile amefunga mabao 19 katika msimu wake wa kwanza wa soka gumu la Misri nadhani tunaweza kusahau kuhusu yeye. Sioni timu ambayo inaweza kumudu kumrudisha nchini.


Kuanzia dau lake la mshahara hadi dau la mauzo ambalo Pyramids itapata akiuzwa. Lakini vilevile kumbuka kwamba kuna ‘signing fee’ kubwa anayoweza kupewa na wakubwa wengine kama wakimhitaji kutoka Pyramids.


Kitu cha kwanza ni kwamba timu aliyokwenda ina pesa za kumbakisha. Lakini kama ikizidiwa pesa basi inaweza kuzidiwa na Zamalek, Waydad Casablanca, Al Ahly, Kaizer Chiefs au Mamelodi Sundowns. Timu gani ya Tanzania ambayo inaweza kutoa dau la Dola4 milioni kwa ajili ya kumchukua Mayele?


Haya mambo tunayasikia kwa wenzetu tu. Bahati mbaya kwetu ni kwamba hilo linaweza kuwa dau la Mayele kwa sasa. Najua kwamba hata mwenyewe anatamani kurudi nchini na kushangiliwa mitaani, lakini hadhi yake imekwenda juu zaidi. Mabao yake yamemchongea.


Kwa Ulaya sidhani kama anaweza kwenda. Ana umri wa miaka 30 kwa sasa. Itakuwa ngumu kwake. Lakini kwa soka la Afrika anaweza kujikuta ameangukia kokote kule kwa wenye fedha ambao mara zote wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la wafungaji.


Udenda unatutoka hasa tunapokumbuka kwamba kuna mastaa wa kigeni wa hapa nchini waliwahi kuondoka halafu wakafeli na kurudi. Waliondoka wakiwa wafalme hasa na tukaombea washindwe katika safari yao ili warudi nchini.


Sala zetu zilitimia kwa Heritier Makambo, Clatous Chama na Luis Miquissone. Hata hivyo, sala zetu hazijatimia kwa Mayele. Ni wazi safari yake ya kurudi nchini inaelekea kuwa ngumu. Labda baada ya miaka mitatu kama moto wake utapungua.


Mayele amenikumbusha mchezaji John Utaka. Wanatofautiana umri tu. Mwaka 2001 Utaka ambaye ni Mnigeria alikuwa anachezea Ismailia ya Misri. Alikuja hapa nchini kucheza na Simba akakabana na Boniface Pawasa. Hata hivyo alionekana kuwa mshambuliaji hatari.


Msimu mmoja baadaye akaibukia zake Lens ya Ufaransa baada ya kufunga mabao ya kutosha pale Misri. Kama Mayele angekwenda Misri akiwa na umri wa Utaka wa wakati ule nadhani naye angepitia njia hiihii kwenda Ulaya.


Na kuna kijana wetu wenyewe. Mbwana Samatta. Alipokwenda TP Mazembe hakurudi. Mpaka leo yupo Ulaya. Alifunga mabao mengi pale DR Congo kiasi kwamba mwishowe alijikuta akicheza KR Genk katika Ligi Kuu Ubelgiji na Ligi ya Mabingwa Ulaya.


Imetokea tena kwa Mayele lakini nadhani ni wakati wa kujiandaa kisaikolojia kwamba Mayele hawezi kurudi tena nchini kirahisi. Hii inakumbusha pengo la walionacho na wasionacho. Sisi bado tunaangukia katika upande wa wasionacho. Hatuna bajeti ya Sh5 bilioni kwa mchezaji mmoja.


Hata hivyo, mpaka sasa hivi tunajitahidi. Walau tuna uwezo wa kutoa Dola 200,000 kumnunua mchezaji. Juzijuzi tu hii ilikuwa bajeti ya klabu kwa msimu mzima. Tumepiga hatua, lakini ukitaka kujua kuwa bado tupo nyuma basi tupige hodi pale Pyramids na kutaka kumrudisha Mayele.


Kinachotoa hofu zaidi ni kwamba sio tu hatuwezi kugonga hodi kumchukua, lakini pia wanaweza kurudi tena nchini na kuamua kumchukua mtu mwingine ambaye wanamtaka. Vipi wakirudi wakamtaka Pacome Zouazoa? Hali inaweza kuwa mbaya kwetu. Hatuwezi kupambana na mshahara wao na wala hatuwezi kuzuia kitita ambacho watatutamanisha.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.