Yanga na Gamondi Ndio Basi Tena, Aamua Kuondoka Akiwa Kifua Mbele



ZANZIBAR; MKATABA wa Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi kuinoa timu hiyo umemalizika, huku akisema hatarajii kuendelea kuwepo klabuni hapo.

Kutokana na hali hiyo kocha huyo amewaaga mashabiki wa timu hiyo na taarifa zinasema huenda akatimkia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, inayotajwa kuwania huduma yake.

Gamondi aliwaaga mashabiki wa Yanga baada ya kumalizika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kati ya Azam FC na Yanga, ambapo Yanga ilitwaa kombe hilo kwa mikwaju ya penalti 6-5, baada ya kumaliza dakika 120 kwa suluhu.

Gamondi amesema ilikuwa mechi ngumu lakini anafurahi kuona timu yake imetwaa kombe hilo na amewashukuru benchi zima la ufundi, mashabiki na wachezaji kwa kipindi chote walikuwa wanatafuta matokeo na kwamba ushindi waliopata maandalizi yake yalianzia mwanzoni mwa msimu.

“Bila maandalizi mazuri tusingepata matokeo mazuri ambayo leo hii yamemfurahisha kila mmoja wetu, nawashukuru kwa ushirikiano mkubwa wa kutusapoti kila tunapokuwepo,” alisema kocha huyo.

Kuhusu kujiunga na timu za Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, kocha huyo alikiri kuwepo na mazungumzo hayo, lakini hakuweka wazi kama ataungana nayo msimu ujao au la.

Amesema yeye ni kocha, anaajiriwa lakini anaweza kuondoka na kwenda timu yoyote ambayo anaona ataweza kufanya nayo kazi, hivyo hajui msimu ujao atakuwa wapi huenda akasalia Yanga pia, ingawa mkataba wake kwa sasa umemalizika.

“Makocha tunaajiriwa ili kufukuzwa, kama nikiondoka hapa naamini nitapata timu nyingine na nitafanya vizuri na kufukuzwa pia, bila kujali nimeondoka vipi,” amesema Gamondi.

Kocha huyo raia wa Argentina, amekinoa kikosi cha Yanga kwa msimu huu wa 2023/24 na amefanikiwa kuipa timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la FA na kuishia hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).

Ukiacha Kaizer Chiefs, Gamondi amesema amepata ofa kutoka nchi mbalimbali za Afrika, hivyo anaamini hata akiondoka Yanga atapata timu nzuri ya kuinoa.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.