SIMBA Washtukia Kamchezo Kachafu, Waamua Kujipanga Upya Kimya Kimya

 

SIMBA Washtukia Kamchezo Kachafu, Waamua Kujipanga Upya Kimya Kimya

UONGOZI wa Simba SC umeshitukia njama zinazoendelea na sasa wameandaa Sera maalum ya kufanya usajili mzuri ili kufanya makubwa kwa msimu ujao kwenye mashindano ya ndani na Kombe la Shirikisho.

Ikumbukwe kuwa misimu mitatu mfululizo Simba imeshindwa kuwa na unyama mwingi kwenye Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho.

Pia imekuwa ikigota hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mfululizo na sasa kumekuwa na sintofahamu katikam uongozi, lakini imebainika Mnyama ameshtuka na anajipanga kimyakimya.

Sera hiyo ambayo Simba imepanga kuja nayo, inaelekeza kuwa usajili wa wachezaji wenye sifa za kuitumikia timu hiyo na si kujaza wachezaji wasiokuwa na tija ambao mwisho wanapata shida katika kuvunja mikataba yao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Simba ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Dk. Seif Muba, amesema;

“Tumeiambia ofisi ya CEO ya Simba itengeneze sera ya usajili ambayo itatumika kusajili wachezaji na kuwaondoa, sera hii itakuwa maalum ambayo tutaitumia wote. Hata ikitokea mimi na wenzangu tukatoka ndani ya uongozi hiyo sera ibaki palepale.”

Katika kukazia hilo, Issa Masoud ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa Fedha Simba na Mjumbe wa Bodi wa klabu hiyo, amesema sio suala la usajili pekee, pia kamati yoyote hata ile ya usajili ambayo inatajwa kuanzishwa, lazima ifuate utaratibu uliopo.

“Jambo lolote linalofanyika ndani ya Simba ambalo haliendani na katiba yetu hilo haliruhusiwi, tumekuwa tukisikia kwamba kuna Kamati ya Usajili imeanzishwa, huo sio utaratibu.

“Kamati yoyote ndani ya Simba inaundwa na Bodi, nje ya Bodi hiyo kamati hatuitambui. Na tumesema sasa hivi hata usajili utakaofanyika nje ya bodi, huo hatuutambui kwa sababu hatutaki kukiuka utaratibu.”

“Kama kuna mchezaji huko atasajiliwa au kocha ataletwa na hajapita katika utaratibu, basi ataenda timu nyingine, hatakuwa ndani ya Simba, hata kama akisajiliwa Cristiano Ronaldo bila ya kupitia kwenye utaratibu wa Bodi atatafuta sehemu ya kuchezea.

“Tumekuwa tukisajili wachezaji wengine wakiwa hawana viwango tunavyovitaka, mwisho wa siku haohao waliomsajili wanakuja kusema mwacheni, akiachwa mchezaji anaacha madeni, klabu imekuwa ikiongezewa madeni yasiyokuwa na vichwa wala miguu. Mwisho wa siku tunatakiwa kufuata utaratibu hata ikitokea kuna deni tunapaswa kulikubali kwani tuliridhia.” CPA Issa Masoud.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.