Sakata la Chama Kwenda Yanga Ngoma Ngumu, Aziz Ki na Dickson Job Wageuka Madalali

Sakata la Chama Kwenda Yanga Ngoma Ngumu, Aziz Ki na Dickson Job Wageuka Madalali


Chama amemaliza mkataba na Simba mwisho wa msimu uliopita, huku mazungumzo ya kumwongezea muda zaidi ndani ya Wekundu hao yakiwa hayana mwafaka zaidi ya kuzua makundi.


Lakini huko Yanga, Mwanaspoti limeambiwa mabosi wa timu hiyo wanapigwa presha na mastaa wakiongozwa na Stephanie Aziz KI na nahodha msaidizi beki Dickson Job ili jamaa asajiliwe na ataongeza kitu msimu ujao.


Inadaiwa Chama ambaye ni raia wa Zambia aliamua kutingisha kiberiti kutaka kusepa Msimbazi, lakini kigogo mmoja anayesimamia usajili wa klabu hiyo akaweka bayana aende tu anakotaka, huku baadhi ya viongozi wengine wakihofia kuuzia silaha adui na kutoelewekwa kwa mashabiki na wapenzi.


Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kwa sasa kuna makundi mawili, la kwanza ni lile lisilotaka kutumia nguvu kubwa kumbakisha Chama, ikiongozwa na matajiri wanaotoa fedha wakitaka atafutwe kiungo mwingine wa maana kwanza.


“Wanaotaka Chama asiongezewe mkataba wanadai amekuwa msumbufu, kwa miaka minne aliyokuwa hapa, lakini hasa hii miwili ya mwisho, wanataka atafutwe kiungo mwingine mwenye makali,” alisema bosi huyo wa ndani ya bodi ya Simba.


Kundi la pili ni lile la wajumbe wapya wa Bodi ya Simba ambao wanataka Chama abakizwe wakati timu mpya inaundwa kisha waje wamteme baadaye timu yao ikiwa vizuri asijue, jambo linaloelezwa limefanya hata Chama kushindwa kutoa uamuzi kama asepe Msimbazi au la akisikilizie kwanza.


Tayari Simba ilishamwekea fedha mezani ambayo akubali au akatae hakuna kitakachoongezeka ikiwa kama mtego kwa kiungo huyo ambaye naye amewawekea ngumu akitaka kiasi hicho kiongezwe.


Tishio kubwa kwa Simba ni vigogo wa Yanga wameingia msituni kimyakimya kumtaka Chama na ameshaweka kiasi kikubwa cha fedha kinachozidi kumtia majaribuni na muda wowote atafanya uamuzi.


Presha kubwa kwa mabosi wa Yanga ni mastaa wa timu hiyo ndio wanaoshinikiza vikali usajili wa Chama wakiongozwa na Stephanie Aziz KI na nahodha msaidizi beki Dickson Job na wengine wakiona kama Mzambia huyo ataongezeka watakuwa na mziki mzito.


Kwa namna dili lilivyokaa kwa sasa ni wazi inasubiriwa kuona kama ni GSM au Mo Dewji na Simba itakayoshinda vita hii ya kiungo huyo aliyemaliza msimu akiwa na mabao saba ya kufungwa na kuasisti saba vile vile wakati Simba ikimaliza nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Azam FC.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.