Ni kweli bado hakijaeleweka. Kiungo mshambuliaji Mzambia, Clatous Chama bado hajamwaga saini ya kuendelea kubali Simba baada ya mabosi wa Msimbazi kushindwa kumtekelezea mahitaji aliyowasilisha mezani ili asalie kikosini.
Ipo hivi. Utata umeibuka ni baada ya mabosi wa Simba kugomea kumuongezea ada ya usajili (sign on fee) ambayo kiungo huyo alikuwa anaitaka ili asaini mkataba wa kuendelea kusalia katika timu hiyo. Simba ni kama imeingia nyongo na Chama ambapo baadhi ya mabosi ndani ya klabu hiyo wakiona Mzambia huyo bado anahitajika, huku kundi lingine lenye nguvu likiona ni bora watengeneze timu mpya itakayokuwa bila ya mchezaji huyo.
Hatua ya pili ambayo Chama na Simba inabishana ni juu ya mshahara ambao anautaka ambao ni sawa au zaidi na ule anaolipwa sasa winga Luis Miquissone. Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, mabosi wa Simba na Chama wameshindwa kuafikiana kwenye dau hilo la mshahara, kwani Mzambia huyo ametaka kulipwa Dola 20,000 (Sh 52 milioni) kwa mwezi.
Kwa sasa inadaiwa, Luis Miquissone ambaye hana namba katika kikosi cha kwanza au kupata nafasi ya kutumika mara kwa mara kikosini, analipwa na Simba zaidi ya Dola 17,000 (Sh 44 milioni) kwa mwezi, mshahara ambao Chama ametaka zaidi ya kiwango hicho ili asaini mkataba mpya na mabosi wa Simba wanaona ni vigumu kumkubalia.
Hatua ya mwisho kwa Simba ni kama kundi linalotaka Chama aachwe linaelekea kushinda kwa vile wao ndio wanaotoa uamuzi makubwa ya bajeti ya klabu hiyo.
Imeandikwa na Mbanga B.