Kocha Minziro Amvulia Kofia Koha wa Yanga Gamondi

Kocha Minziro Amvulia Kofia Koha wa Yanga Gamondi


Kocha wa Kagera Sugar, Fred Felix 'Minziro' amesema ubora wa wachezaji wa Yanga ndio uliamua mechi ya juzi ambayo walipoteza kwa bao 1-0.


Minziro alisema Yanga wana wachezaji wenye ubora mkubwa ambao wanaweza wakabadilisha matokeo muda wowote ndio sababu pamoja na timu yake kucheza vizuri na kuwabana wapinzani wao bado walitumia vyema kosa moja walililofanya wachezaji wake.


"Ubora wa wachezaji wa Yanga uliamua mechi, tulicheza vizuri muda mwingi wa mchezo lakini kosa moja tulilolifanya walituadhibu, kwangu mimi naona ni ubora wa wachezaji tu umeamua mechi, tulicheza vizuri na nawapongeza wachezaji wangu kwa kucheza vizuri," alisema Minziro.


Alisema dakika za mwisho kulikuwa na umakini mdogo kwa safu yake ya ulinzi na kupelekea yanga kutumia makosa hayo kupata goli lililofungwa na kiungo Mudathir Yahaya.


"Mabeki walichelewa kufika kwenye nafasi kwa haraka na kumpa nafasi Mudhathir kutuadhibu, hata hivyo mchezo huu umepita tunajipanga kwa ajili ya mchezo mwingine wa mbele yetu," alisema Minziro.


Alisema wanapaswa kupambana katika michezo iliyobakia ili kuweza kujiondoa kwenye nafasi waliyopo sasa na kupanda juu kabla ya kujua hatima yao mwishoni mwa ligi.


Kagera Sugar inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na pointi 30 baada ya kucheza michezo 26, hata hivyo imezizidi michezo miwili timu mbili za chini yake, JKT Tanzania na Singida Big Stars ambazo zote zina pointi 29.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.