GARI Limewaka, Sijaona cha Kuizuia Yanga Ubingwa Ligi Kuu

Kikosi cha Yanga


Kimahesabu ya kimpira, mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara zilikamilika siku ile ambayo Simba ilipoteza kwa mabao 2-1 mbele ya Yanga katika mechi ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo.


Isingekuwa rahisi kwa Simba na Azam kuifikia Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi kutokana na sababu mbalimbali japo zenyewe zikawa zinajifariji kwamba zinaweza kufanya hivyo.


Simba ilikuwa na matumaini ya kufuta pengo la pointi nane na kuipiku Yanga lakini kiuhalisia kwa ubora wa timu nyingi za Ligi Kuu na kile kinachoonyeshwa na Yanga uwanjani, isingekuwa rahisi kwao kupoteza mechi mbili au tatu ambazo zingefanya wafikiwe na kupitwa.


Ni kama ambavyo ilivyokuwa kwa Azam FC kwamba ingeweza kupata ushindi katika mechi zake lakini je nani ataifunga Yanga kengele?


Jambo gumu zaidi kwa Simba na Azam ni kwamba zina mchezo ambao utazikutanisha zenyewe hivyo mmojawapo au zote zitakuja kuangusha pointi na hivyo kuipunguzia Yanga kazi katika kibarua cha kusaka ubingwa.


Halafu pia timu kama Simba ndani ya uwanja sasa hivi imekuwa haina makali kiasi ambacho haitoi uhakika kama inaweza kupata ushindi katika mechi zake zote ambazo zimebakia ili tuone hayo maajabu ya kuipiku Yanga kama nayo itapoteza.


Ukiangalia kwa Azam FC ina mechi nne kati ya sita zilizobaki ambazo itacheza ugenini mahali ambako imekuwa haitishi sana wala kuwa na takwimu nzuri za kufumania nyavu.


Uzuri wa Azam FC ni kama walishtukia mchezo wakaanza kujiimarisha katika kusaka nafasi ya pili ili hata wakikosa ubingwa angalau waangukie hapo wacheze Ligi ya Mabingwa Afrika.


Kwa Yanga, kilichobakia ni kukamilisha tu taratibu za kimpira lakini tusiaminishane kuwa lolote linaweza kutokea wakakosa ubingwa, japo mpira una maajabu.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.