Kiungo wa Klabu ya Yanga, Pacome Zouzoua, ataendelea kukosekana katika mchezo wa leo dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Pacome anaendelea kukosekana baada ya kutokuwa fiti kuanza kucheza kutokana na majeraha yaliyokuwa yakimsumbua.
Kiungo huyo raia wa Ivory Coast, aliumia Machi 17, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Azam, tangu hapo hadi leo hajacheza mechi yoyote.
Daktari wa Young Africans SC, Moses Etutu, amesema Pacome hatocheza leo, lakini baada ya mchezo huu ataanza mazoezi ya pamoja na wenzake kujiandaa na mchezo unaofuata.
“Pacome atakosekana leo, lakini baada ya hapa, ataanza mazoezi na wenzake kujiandaa na mchezo unaofuata wa Robo Fainali ya CRDB Federation Cup dhidi ya Tabora United,” alisema Etutu.
Mchezo wa leo utakuwa ni wa saba mfululizo kukosekana kwa Pacome uwanjani tangu aumie Machi 17, mwaka huu.