Yanga Vs Mamelodi kuna bato ya vigogo vijana

Yanga Vs Mamelodi kuna bato ya vigogo vijana


Mchezo huo wa kwanza baadaye utafuatiwa na mechi ya marudiano itakayopigwa pale Loftus Versfeld jijini Pretoria nchini Afrika Kusini, Aprili 5, itakayoamua timu ipi itatinga nusu fainali ili kuvaana na mshindi wa mechi nyingine ya robo fainali kati ya Esperance ya Tunisia na Asec Mimosas ya Ivory Coast.


Presha ya mchezo huo inazidi kuwa kubwa wakati ikisubiriwa Mamelodi ambayo inaelezwa itatua nchini leo Alhamisi, lakini nje ya mechi hiyo kuna vita ya kibabe ya vigogo wawili vijana wanaoziongoza klabu hizo.


Wenyeji Yanga, klabu yao iko chini ya Rais Hersi Said ambaye ndiye mtu aliyesimama nyuma ya mafanikio ya mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara kwa kipindi cha miaka mitatu.


Hakuna mchezaji aliyepo katika kikosi hicho hajapitia kwenye mikono ya Hersi kuanzia usajili mpaka sasa alipo ndani timu hiyo.


Maisha hayohayo amekuwa nayo pia Tlhopie Motsepe ambaye ni Mwenyekiti wa Mamelodi akichukua kiti hicho kutoka kwa baba yake, Dk Patrice Motsepe, ambaye aliona klabu hiyo itakuwa kwenye mikono salama mbele ya kijana wake huyo wa kiume aliyekuwa karibu naye wakati akiwa klabuni hapo.


HERSI FAINALI, TLHOPIE BINGWA AFL


Hersi ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Afrika, rekodi kubwa ambayo anatamba nayo ni kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo Yanga ilicheza kwa mara ya kwanza msimu uliopita ikiwa ni rekodi kubwa ya klabu hiyo.


Upande wa pili, mwenzake Tlhopie amefanikiwa kuweka kabatini ubingwa wa African Football League ikiwa ni klabu ya kwanza kuchukua ubingwa huo wa mashindano hayo makubwa ya klabu yaliyoanza mwaka jana.


USHAWISHI KWA WACHEZAJI


Hersi na Tlhopie kila mmoja akiwa klabuni kwake wamekuwa wakijitambulisha kwa kuishi karibu na wachezaji wa timu zao, kila mmoja amekuwa na nguvu yake katika ushawishi wa kutafuta matokeo na hata rekodi mbalimbali za klabu zao hizo mbili jambo ambalo limewajengea imani kubwa na wachezaji kuzipigania klabu hizo uwanjani.


Hersi na GSM, Tlhopie na Motsepe


Huwezi kumtofautisha Hersi na Ghalib Said Mohammed ambaye amekuwa mfanikishaji wa karibu kila kitu kuhusu jeuri ya Yanga kifedha kuanzia usajili mpaka maisha mengine ya gharama kubwa.


Vivyo hivyo kwa Tlhopie naye amekuwa na nguvu kubwa na klabu yao kutokana na nguvu ya kifedha ya baba yake ambaye ni tajiri mkubwa wa biashara ya madini nchini Afrika Kusini.


Mamelodi imekuwa na nguvu ya kusajili mastaa ghali kutoka nje ya Afrika kutokana na ukwasi wa Motsepe ambaye yumo kwenye orodha ya matajiri 10 bora wa Afrika.


WAZEE WA PAMBA


Hersi na Tlhopie wote ni vijana, kila mmoja amekuwa maarufu eneo lake kutokana na mwonekano wa mavazi yao. Ilizoeleka watu wa nafasi zao huko nyuma kuwaona wanavaa mavazi ya suti kila wakati, lakini kwa vijana hawa wawili ni tofauti.


Wakati Hersi anaingia madarakani ilikuwa ikielezwa viongozi wanaovaa suruali aina ya jeans zilizotoboka itakuwa vigumu kuipa klabu hiyo matokeo, lakini mpaka sasa amekuwa akijitambulisha kwa mafanikio makubwa bila kuwa na anguko.


Vivyo hivyo kwa Tlhopie, kwani ukimkuta katika maeneo yake ya kujidai unaweza kubisha kwamba si mwenyekiti wa klabu hiyo, kwa umri alionao na hata mavazi yake ya ujana wote wakiwa nadhifu miilini lakini pia smati vichwani.


Jumamosi hii wote watakuwa katika jukwaa kuu la Uwanja wa Mapa wakiziongoza klabu zao kupambana kwa mara ya pili katika historia ya timu hizo, lakini safari hii zikiwa na viongozi vijana. Acha tukaone vita ya kibabe.


Mara ya kwanza kwa timu hizo kuvaana ilikuwa katika mechi za raundi ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2001, ambapo Mamelodi ilishinda kwa mabao 3-2 nyumbani kisha kupata sare ya mabao 3-3 ugenini na Yanga kuaga michuano kwa kipigo cha jumla cha mabao 6-5.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.