Kesho Yanga itaikaribisha Mamelodi Sundowns kwenye mechi ya timu mbili zenye uwezo tofauti wa kiuchumi.
Uwekezaji kwenye kikosi cha Mamelodi si sawa kabisa na Yanga, kuna pengo kubwa baina yao, lakini waswahili wanasema hivi, pesa hainunui mapenzi.
Kwa maana kwamba, uwekezaji unaweza kuwa mkubwa, lakini usikupe matokeo. Soka linaamriwa kwa kiwango cha siku husika ya mchezo. Ngoja tuone, itakuwaje Kwa Mkapa hiyo kesho?
Mamelodi thamani yao ni kubwa. Yanga inaonyeshwa kuwa na thamani ya Euro 1.85 milioni sawa na Sh3 Bilioni wakati kiungo mwenye thamani kubwa zaidi ndani ya Mamelodi ni Marcelo Allende sawa Euro 2.30m kama Sh6 Bilioni.
Nyuma ya Allende ambaye ni raia wa Chile wamo Matias Esquivel na mshambuliaji Peter Shalulile wenye thamani ya Euro 2.20 milioni ambazo ni sawa na Sh5.5 bilioni.
Pale Yanga wao mtandao huu unawaonyesha wachezaji ghali ni kiungo wao mshambuliaji Stephanie Aziz KI na beki Lomalisa Mutambala wakiwa ndio wachezaji wenye thamani kubwa ya Euro 250,000 kila mmoja ambazo ni sawa na Sh689 milioni kwa kila mmoja.
Hata hivyo, mtandao huo unaoaminika kwa kufanya makadirio duniani haujaweka taarifa za vikosi vizima vya Simba na Yanga kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mastaa wake kutotambulika zaidi kimataifa.
Kocha na Mchambuzi wa soka, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’, alikiri Yanga kuzidiwa kiuchumi na Mamelodi lakini akasema soka linapigwa uwanjani na sio mfukoni.
“Ni kweli pesa inaongeza kitu na ubora kwenye timu lakini mechi moja inategemea dakika 90 za uwanjani. Hapo ndipo mechi inachezwa hivyo unakuta mchezaji ghali anakabana na mchezaji wa kawaida na mwisho wa siku anashinda huyo wa kawaida, hivyo hilo lisizitishe timu zetu za Tanzania,” alisema Mzazi.
Mchambuzi wa Soka, George Ambangile alisema soka linachezwa uwanjani na timu iliyojiandaa vizuri ndiyo inashinda.
“Pesa ni muhimu sana kwenye mchezo lakini ni tofauti na uhalisia. Unaweza kusajili mchezaji kwa pesa nyingi lakini asikupe kitu ulichotarajia na mara nyingine akawa wa kawaida, mifano ipo mingi duniani na hata kwenye maisha ya kawaida. Pesa nyingi sio kigezo cha ufanisi uwanjani,” alisema Ambangile.
Kiungo wa zamani wa Taifa Stars, Amri Kiemba alisema bila kujali pesa, timu yoyote ya mpira inaweza kushinda na kushindwa.
“Kila timu ya soka inashinda na kushindwa na hiyo ndio raha ya mchezo huu hivyo pesa inasaidia katika mambo mengi lakini sio kigezo ukiweka pesa nyingi basi utashinda kila mchezo,” alisema Kiemba ambaye ni mchambuzi wa soka.