Siku nane za moto kwa Moallin KMC

Siku nane za moto kwa Moallin KMC


Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moalin amesema ana siku nane za moto kabla ya kuikabili Tanzania Prisons aliyokiri imeimarika chini ya Hamad Ally akitaka kutibua rekodi aliyonayo tangu ajiunge na maafande hao.


KMC iliyopo nafasi ya sita ikikusanya pointi 28 katika mechi 21 itakuwa ugenini Aprili 12 kuvaana na Tanzania Prisons iliyo nafasi ya tano na ikilingana nao pointi ila zikitenganishwa kwa mabao ya kufunga na kufungwa. Hata hivyo mechi hiyo itapigwa baada ya KMC kumalizana na Ihefu kataika mechi ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) itakayochezwa Aprili 6 jijini Dar es Salaam.


Akizungumza Moallin alisema wanatambua ubora wa Prisons chini ya kocha Hamad aliyewahi kuinoa KMC, lakini hilo haliwatishi kwani hata wao wana malengo makubwa ya kuhakikisha wanakusanya pointi kwa kila mchezo ulio mbele yao ili kuweza kufikia malengo ya kumaliza tano bora.


"Tumesharudi mazoezini na timu inaendelea vizuri ipo kwenye morali nzuri kuhakikisha inakusanya pointi kwenye kila mchezo ulio mbele yetu mbinu sahihi na maandalizi mazuri yatatupa nafasi ya kuwa bora zaidi ya mpinzani wetu," alisema Moallin aliyewahi kuinoa Azam FC na kuongeza;


'Prisons tangu imemkabidhi timu kocha wao mpya imebadilika aina ya uchezaji na imekuwa bora maeneo mengi hilo tayari tumeanza kulifanyia kazi kwa kutafuta mapungufu yake na kubaini ubora wao ili tujue namna ya kumzuia."


Moallin alisema anaimani kubwa na kikosi chake, licha ya mechi za karibuni kushindwa kuwa na matokeo mazuri amefanyia kazi makosa aliyoyaona sasa anapambana kusuka mbinu za kumfunga Tanzania Prisons.


Mechi tano za hivi karibuni kwa makocha hao Prisons inaonekana kuwa bora zaidi, kwani imefungwa mchezo mmoja sare mbili na kushinda mechi mbili, wakati kwa Moallin kakubali kichapo kimoja, ushindi mara moja na kutoka sare mechi tatu wote wamecheza mechi 21 na kukusanya pointi sawa tofauti ni mabao ya kufunga na kufunwa.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.