Mkude amficha kiungo wa bilioni 6 Mamelodi

Mkude amficha kiungo wa bilioni 6 Mamelodi

Kiungo Jonas Mkude 'Nungunungu' jana usiku alikuwa anafanya kazi chafu kwenye eneo la kiungo cha Yanga kiasi cha kumpa wakati mgumu fundi wa Mamelodi Sundowns, Marcelo Allende anayetajwa kuwa na thamani ya Euro 2.30 milioni (zaidi ya Sh6 bilioni) katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa.


Kocha Miguel Gamondi, ni kama aliwasapraizi mashabiki kwa kumuanzisha kiungo huyo wa zamani wa Simba katika nafasi ya Khalid Aucho aliye majeruhi, kwani hakuna aliyekuwa akitegemea kama angeanzishwa, lakini alivishwa mabomu naye akajituma kuonyesha uzoefu alionao ni hazina tosha kwa mechi kama hizo.


Mkude ambaye alikuwa akishirikiana na Mudathir Yahya, aliifanya Yanga kuwa na utulivu kwenye eneo hilo huku akirahisha mashambulizi kutokana na kuachia kwake mpira kwa haraka kwa pasi fupifupi na ndefu ilipohitajika.


Viungo wa Mamelodi wakiongozwa na Allende walikuwa na wakati mgumu kupita eneo hilo kiasi cha mara nyingi kuonekana wakitengeneza mashambulizi yao wakipitia maeneo yao ya pembeni ambayo walikuwa wakitumika zaidi mabeki wao, Khuliso Mudau na Divine Lunga.


Akiongelea kiwango cha Mkude, Miguel Gamondi, alisema, "Niliamini kuwa anaweza kufanya vizuri kwenye eneo hilo kulingana na maandalizi ambayo tulifanya na sikuwa na shaka na hilo na kiukweli niwapongeze wachezaji wangu wote kwa kazi nzuri ambayo wameifanya, bado tuna dakika 90 nyingine."


Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Mkude kucheza kwa dakika 90 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Yanga, ikumbukwe kuwa kiungo huyo ana uzoefu wa kutosha na michuano hiyo kwani wakati akiwa na Simba alicheza kwa zaidi ya msimu mitatu tofauti na kufika hatua kama hii ya robo fainali.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.