Kumbe Anayemwaribia Fiston Mayele Huko ni Huyu Mwamba, Hakuna cha Majini Wala Nini..........

Kumbe Anayemwaribia Fiston Mayele Huko ni Huyu Mwamba, Hakuna cha Majini Wala Nini..........


Straika wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele amekuwa gumzo kutokana na ‘ligi ndogo’ aliyoianzisha na mashabiki wa klabu hiyo juu ya kushuka kwa kiwango alicho nacho katika timu ya Pyramids, hata hivyo imebainika mdudu anayemkwamisha Mkongomani huyo kushindwa kuwika katika timu hiyo tofauti na alivyokuwa Jangwani.

Mayele aliyeitumikia Yanga kwa misimu miwili na kutwaa nayo ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii na Kombe la ASFC mara mbili mbili na kucheza pia fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ameanzisha malumbano na wana Yanga kutokana na kushindwa kuwika Pyramids, lakini imebainika ‘mchawi’ anayemtibulia nyota huyo wala sio wana Jangwani.

Ushindani wa namba baina yake na Msauzi, Fagrie Lakay ndio unaoelezwa kumkwamisha Mayele kulinganisha na alivyokuwa Yanga alipojitengenezea ufalme kikosi hadi anapoondoka kwenda Misri kujiunga na Pyramids.

Katika mashindano yote, Mayele ambaye ametumika katika dakika 1,153 amehusika katika mabao matano tu, manne ya Ligi ya Misri huku moja likiwa upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Pyramids FC imeishia hatua ya makundi.

Kwa upande wa mchezaji anayechuana naye kwenda eneo hilo la ushambuliaji la Pyramids, Lakay ametumika katika dakika 1,416, amehusika katika mabao saba, akifunga matano yakiwamo mawili katika Ligi Kuu ya Misri na mawili mengine ya Kombe la Ligi, huku akitupia poa moja la Ligi ya Mabingwa Afrika akitoa pia asisti mbili.

Mayele aliyekuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara (17) msimu uliopita akiwa akilingana na Saido Ntibazonkiza wa Simba, lakini akitupia saba kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kuanzia makundi hadi fainali, huku kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na play-off ya Shirikisho alifunga jumla ya mabao saba pia.

Wakati anasajiliwa Pyramids alimkuta Lakay kikosini ambaye naye takwimu zake zinaonyesha alifunga mabao 12 katika mashindano yote, huku akitoa asisti nne.

TATIZO LILIANZIA HAPA

Mayele alisajiliwa na Pyramids na Kocha Jaime Pacheco aliyevutiwa na umahiri wa straika huyo wa zamani wa AS Vita, akiamini mshambuliaji huyo anaweza kuongeza makali kwenye kikosi hicho, lakini mabadiliko ya benchi la ufundi yamewafanya washambuliaji hao wote kuwa na nafasi sawa kwenye kikosi hicho.

Kocha Pacheco alifutwa kazi Februari 5 mwaka huu na hapo ndipo balaa likaanza kwani kocha aliyekuwa kuchukua nafasi hiyo, ameuacha mlango wazi kwa wachezaji wote, kila mmoja apambane na hali yake ili amvutie kikosini na hapo, ndipo Mayele akaanza kupaa kibarua.

Mayele ametakiwa kumthibitishia kocha mpya wa kikosi hicho, Krunoslav Jurcic kuwa anastahili nafasi ya mara kwa mara kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Kocha huyo mpya wa Mayele, amezinoa klabu mbalimbali kubwa barani Ulaya ikiwemo Dinamo Zagreb ya nyumbani kwao Croatia, NK Maribor ya Slovenia, Adanaspor ya Uturuki na Al-Nassr ya Saudi Arabia ambayo kwa sasa anaichezea Cristiano Ronaldo amewaachia kila mchezaji kukomaa ili apate nafasi.

NINI AFANYE?

Kutokana na hali aliyokumbana nayo nyota huyo kwa sasa tofauti na alivyokuwa Yanga, ni lazima aiache miguu yake ifanye kazi badala ya kutafuta wa kumtupia lawama, kwamba anaobishana nao wanachangia kumfanya asiendelee kuwika.

Mayele ana kitu cha kujifunza kutoka kwa nyota wengine waliowahi kuwika Ligi Kuu Bara kabla ya kwenda kuchemsha katika timu za Arabuni kama ilivyowahi kumtokea Clatous Chama na Luis Miquissone, waliowika Simba misimu miwili iliyopita, lakini wakikwama kujitengenezea ufalme katika klabu za RS Berkane ya Morocco na Al Ahly ya Misri.

Chama aliuzwa Berkane sambamba na Tuisila Kisinda, lakini alijikuta akichemsha na kurejea Simba baada ya nusu msimu, huku Luis alishindwa kupenya kikosi cha kwanza cha Al Ahly na kutolewa kwa mkopo timu nyingine za huko kabla ya kurejea Msimbazi ambapo bado anaendelea kujitafuta.

Pia ni lazima atambue anacheza na wachezaji tofauti na wale aliowazoea akiwa Yanga ambao walikuwa wakimlisha mipira na kumtengenezea nafasi mbali na zile alizozitengeneza mwenyewe na kumfanya awe tishio kwa mabeki na makipa wa timu pinzani, hivyo hata huko akiendelea kuzoeleka Pyramids atakuwa na moto uleule wa zamani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.