Klabu zingine zijifunze kwa Tabora United

Klabu zingine zijifunze kwa Tabora United


Timu hiyo inayocheza ligi hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kupata daraja kutoka Ligi ya Championship ikitumia jina la Kitayosce, hadi sasa ipo nafasi ya 13 katika msimamo baada ya kucheza mechi 21 na kuvuna pointi 21 tu ikiwa wastani wa kila mechi imepata pointi moja tu.


Nafasi iliyopo na wastani wa pointi inayovuna katika kila mechi kwa idadi ya michezo iliyosalia (9) ni lazima ifanye kazi ya ziada ili kuijihakikisha inasalia ndani ya ligi hiyo kwa msimu ujao.


Inatakiwa kupigana kufa au kupona kupigania kubaki katika hadhi hiyo waliyoipigania kwa gharama hadi kusababisha kiongozi kupewa adhabu ya kufungiwa kutokana na tuhuma za rushwa ya kupanga matokeo.


Timu hiyo inayotokea Tabora ilikuwa na makali Ligi Daraja la Kwanza (sasa Championship) na ilianza kuonja shubiri ya Ligi Kuu baada ya kuzuiwa na Shirikisho la soka la Kimataifa (Fifa), kutumia baadhi ya wachezaji wake kutokana na kudaiwa na kocha wake wa zamani.


Kutokana na katazo la Fifa, timu hiyo ikacheza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC ikiwa na idadi ya wachezaji wanane, hivyo mchezo kuisha baada ya wachezaji kuumia na timu kubaki na idadi chini ya wachezaji saba wanaoruhusiwa kwenye mchezo. Matokeo yakawa ni kufungwa mabao 4-0.


Upepo mbaya walioanza nao Tabora hauonekani kutulia huku ligi ikiwa imeanza raundi ya pili; sasa timu hiyo inakabiliwa na tishio la kukimbiwa na wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi wa sekretarieti.


Inaonekana fedha linaenda kuwa tatizo linaloweza kusiriba hatima ya Tabora Ligi Kuu.


Kwa maneno ya mchambuzi maarufu wa soka wa Dar es Salaam; “Klabu ya Ligi Kuu inaishi maisha ya klabu ya Daraja la Nne.”


Tatizo sio hilo tu kwa ‘Nyuki’ hao wa Unyanyembe, rungu la Fifa pia linaweza kuwagonga kiasi cha timu kutoweka kabisa katika vitabu vya mpira.


Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu, Thabit Kandoro tayari ameshakabidhi barua ya kujiuzulu akielezea ukata ambao umefikia kiasi cha kuathiri ufanisi wa timu.


Iwapo hali itaendelea hivyo, wote wenye mikataba na ambao hawajatimiziwa matakwa yao wanaeza kuondoka huku wakiacha nyuma mzigo wa madai ya fidia ambayo klabu haiwezi kuzilipa.


Hadi sasa hivi kuna maswali hayajapata majibu kuhusu Tabora United, mfano, nini chanzo cha mapato cha timu hii? Nani anaimiliki?


Ni mali gani zinamilikiwa na klabu hiyo? Maswali haya yanaenda pia kwa klabu nyingi za Ligi Kuu. Unajiuliza klabu kama Tabora inatoa wapi ubavu wa kusajili wachezaji 12 wa kigeni?


Ni nani ana dhamana ya hizi timu iwapo zitashindwa kulipa madeni ya mishahara, huduma na bidhaa wanazonunua? Utaratibu wa Leseni za Klabu kweli unatumika sawa ili kuona kwa uwazi vyanzo vya mapato vya klabu?


Inashangaza kuona klabu ambayo haiwezi kulipa mishahara ya wachezaji inapigana vikumbo vya usajili na klabu zenye mafungu makubwa ya fedha kama Yanga, Simba na Azam.


Kibiashara ni jambo jema kuona klabu zinajitahidi kuwekeza na kununua wachezaji, makocha na hata watumishi wengine kutoka kona mbalimbali za dunia.


Hata hivyo, ni muhimu na busara pia uwekezaji huo usizidi uwezo wa klabu kutimiza majukumu yake ya kifedha kama mmiliki na mwajiri.


Ni kweli klabu zinataka kununua mafanikio, lakini unahitajika weledi sana katika matumizi ya fedha.


Katika miaka ya mwisho ya 1990 hadi mwanzoni mwa 2000, klabu ya Leeds United ya England ilipata mafanikio katika Ligi ya Uefa na ile ya Mabingwa wa Ulaya kwa kufika nusu fainali.


Kwa timu hiyo ambayo hata haikuwa bingwa wa nchi, hayo yalikuwa mafanikio makubwa, pia iliingiza pesa nyingi.


Kilichofuata ilikuwa ni timu kuwekeza zaidi katika kununua wachezaji ili iendeleze mafanikio hayo au iende mbele zaidi.


Kilichokuja kutokea ni klabu kujikuta katika mzigo wa madeni ulioilazimisha kuuza wachezaji wengi wazuri na huo kuwa mwanzo wa mwisho wa mafanikio.


Klabu iliuza wachezaji mahiri kama Rio Ferdinand aliyekwenda Manchester United kwa kitita cha paundi zipatazo milioni 30.


Ikamuuza Jonathan Woodgate ambaye mwenyekiti Peter Ridsdale alikuwa ameapa kwamba hatamuuza. Baada ya mambo kuwa magumu, mwenyekiti mwenyewe akabwaga manyanga na timu kuongozwaa na mwanachama Mackenzie ambaye hakudumu sana, kwani timu iliwekwa chini ya ufilisi na ukaanza mchakato wa kupata wawekezaji wapya.


Leeds iliendelea kushuka na kushuka kwa miaka kadhaa hadi ikafika Daraja la Tatu ikiwa na hali mbaya iliendelea hivi karibuni ilipofanikiwa kurejea katika Ligi Kuu na kushuka tena daraja inakofanya vizuri.


Kisa cha Leeds United ni kirefu sana kusimulia, lakini ndiyo hali inavyoweza kuwa kwa klabu zinazokuwa na tamaa ya kununua mafanikio. Bahati mbaya kwa mpira wetu, hakuna sheria za mpira au za serikali zinazoweza kudhibiti matumizi au kuweka njia za kuisaidia timu inayopitia katika mazingira wanayopitia Tabora.


Niliongea na mkongwe mmoja wa mambo ya utawala wa mpira wa miguu anasema kuwa mpira wetu unakwenda halijojo, hasa linapokuja utawala wa klabu.


“Hizi klabu hazina mipango mkakati, hakuna kanuni za fedha wala miongozo ya raslimali watu. Bado klabu zetu zinaendeshwa kienyeji mno,” anamalizia mkufunzi huyo wa utawala anayetambuliwa na Fifa.


Ligi yetu inatajwa kuwa miongoni mwa ligi tano bora barani Afrika. Binafsi sijui vigezo hasa vinavyotumika kujua ligi kuwa ni bora au la. Inawezekana ligi ikatoa klabu zinazofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, hilo ni jambo jema.


Jambo la hatari ni pale katika ligi hiyo kutakuwa na timu itakayoshindwa kusafiri ili kutimiza majukumu yake ya kimashindano. Pia ni hatari kama timu itazuiwa kusajili kwa sababu ya madeni yake kwa wachezaji na watumishi wengine. Sio afya kwa ligi kwa sababu mwishowe timu zitashindana katika uga usio sawia. Mfano, angalia mchezo wa kwanza wa Azam dhidi ya Tabora, wageni hao walifungwa wakiwa pungufu na katika mchezo wa marejeano timu hizi zinatoshana nguvu kwa kutoka suluhu.


Matokeo ya mchezo huo yanaweza kuamua bingwa au timu ya kushuka au mfungaji bora wa ligi. Kwa hali hiyo kuna umuhimu wa kuangalia afya za klabu ili iwe chachu ya kuboresha ligi.


Fedha ni muhimu katika kuendesha timu, lakini weledi ni muhimu zaidi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.